CR7 kufungua baa, hoteli huko England
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 41, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Ligi Kuu Saudi Arabia, Al-Nassr, anaripotiwa kupanga kufungua kumbi nchini England wakati atakapostaafu soka la kulipwa.
LONDON, ENGLAND: SUPASTAA Cristiano Ronaldo amefichua mpango wake wa kupanua biashara yake ya hoteli na baa huko England.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 41, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Ligi Kuu Saudi Arabia, Al-Nassr, anaripotiwa kupanga kufungua kumbi nchini England wakati atakapostaafu soka la kulipwa.
Ronaldo, maarufu kama CR7 na shujaa wa zamani wa Manchester United, alisaini makubaliano mwaka 2016 na mnyororo wa hoteli wa Ureno Pestana Hotel Group kwa ajili ya hoteli na baa zenye chapa ya Ronaldo.
Ushirikiano huo, unaoendesha kumbi za Inverse by Pestana CR7 kote Ureno, umeomba kusajili alama ya biashara nchini England.
Chanzo kimoja kilisema: “Cristiano hufanya maamuzi ya kibiashara kwa busara. Wachezaji wengine wa soka wameonyesha kuwa ni soko lenye mafanikio. Ana fedha na taswira ya kuweza kuwazidi wote.”
Ronaldo, anayejulikana kwa kuzingatia sana mazoezi ya mwili, hajaonyesha ni lini ataacha soka la kulipwa, lakini upanuzi wake mkubwa wa biashara unaweza kuwa ishara kwamba anajiandaa kwa maisha baada ya soka.
Chanzo kingine kilisema: “Cristiano ni mtu mwenye akili na hufanya maamuzi sahihi ya kibiashara.
“Bado anapendwa sana Manchester na anajua kuna soko kwake endapo angependa kufungua baa.”
Mchezaji mwenzake wa zamani katika klabu ya Manchester United, Gary Neville, anaendesha Hotel Football karibu na Uwanja wa Old Trafford.