CR7 amchumbia demu wake baada miaka tisa
Muktasari:
- Mrembo Georgina, 31, alifichua hilo baada ya kuposti kwenye Instagram picha ya mkono wake akiwa na pete kubwa ya uchumba kidoleni.
LISBON, URENO: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo hatimaye amemchumbia mpenzi wake wa muda mrefu, mrembo Georgina Rodriguez.
Mrembo Georgina, 31, alifichua hilo baada ya kuposti kwenye Instagram picha ya mkono wake akiwa na pete kubwa ya uchumba kidoleni.
Wapendanao hao wamekuwa pamoja kwenye uhusiano kwa kipindi cha miaka tisa, lakini huko nyuma, Ronaldo alikuwa akisitasita kumchumbia mrembo huyo.
Kuthibitisha hilo, mrembo Georgina aliposti mkono wake wenye kidole cha pete ya uchumba huku ukiwa juu ya mkono wa Ronaldo.
Kinda mrembo huyo mwanamitindo aliandika: "Ndiyo, nimekubali. Kwenye hili na maisha yangu yote."
Mrembo Georgina amekuwa akiamsha uvumi wa kuchumbiwa tangu Aprili mwaka huu wakati alipokuwa akiposti picha za pete tofauti kwenye kidole chake. Desemba mwaka jana, wakati alipohudhuria tuzo za Globe Soccer Awards huko Dubai, Ronaldo alichanganya ulimi aliposema: "Ni furaha kubwa kushinda tuzo hii. Mwanangu mkubwa yupo hapa na mke wangu (Georgina) yupo pia."
Huko nyuma alipobainisha kwanini hajamuoa mpenzi wake wa muda mrefu, Ronaldo, 40, alisema: "Siku zote nimekuwa nikimwambia, 'tutalifanya hilo tutakapoelewana zaidi.' Kama vile kufahamiana vyema maisha yetu na yeye anafahamu vyema ninachokizungumzia.
"Inaweza kuchukua mwaka au miezi sita au mwezi. Nina uhakika kwa asilimia 1,000 hilo litatokea."
Mrembo Georgina, kwa upande wake alisema kuhusu marafiki zake: "Siku zote wamekuwa wakinitania kuhusu harusi. 'Harusi ni lini?'
"Tangu wimbo wa Jennifer Lopez wa 'The Ring Or When' ulipotoka, wameanza kuniimbia. Na nawaambia, huo si uamuzi wangu."
Ronaldo na Georgina wamefanikiwa kupata watoto wawili wa kike, Alana, 7, na Bella, 2, wakati Bella pacha wake Angel, alifariki wakati anazaliwa.
Mrembo Georgina pia amekuwa akimsaidia Ronaldo kuwalea watoto wake wengine watatu ; Cristiano Jr, 15, Mateo, 8, na Eva Maria, 8.
Wawili hao walikutana 2016, wakati mrembo Georgina alipokuwa akifanya kazi kwenye duka la Gucci huko Madrid.