Courtois amkosoa Jose ishu ya Vini
Muktasari:
- Vinicius Jr alifunga bao pekee la mchezo wakati Real Madrid na Benfica zilipokutana katika mechi ya mkondo wa kwanza ya mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki iliyopita.
MADRID, HISPANIA: KIPA, Thibaut Courtois amekuwa mtu mwingine wa hivi karibuni kukosoa kauli zilizotolewa na Jose Mourinho kuhusu ushangiliaji wa Vinicius Junior dhidi ya Benfica. Kipa huyo wa Real Madrid alisema hafurahishwi kuona ushangiliaji huo ukitumiwa dhidi ya mwenzake, hasa baada ya kudaiwa kufanyiwa ubaguzi wa rangi.
Vinicius Jr alifunga bao pekee la mchezo wakati Real Madrid na Benfica zilipokutana katika mechi ya mkondo wa kwanza ya mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki iliyopita.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil alidai kuwa alitukanwa kwa misingi ya rangi na Gianluca Prestianni wakati wa mchezo huo, ambao ulisimamishwa kwa dakika 10 huku nyota huyo wa Real Madrid akiondoka uwanjani kufuatia tukio hilo.
UEFA imeanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma hizo na Prestianni amesimamishwa kwa muda wakati uchunguzi ukiendelea, hatua inayomfanya akose mechi ya marudiano wiki hii.
Kocha wa Benfica, Mourinho, alisema Vinicius Jr aliwachochea mashabiki kwa ushangiliaji wake wa bao baada ya mchezo wa wiki iliyopita. Hata hivyo, Courtois amepuuza kauli hizo, akisisitiza kuwa hilo haliwezi kutumika kuhalalisha ubaguzi wa rangi.
“Mourinho ni Mourinho na kama kocha daima utailinda klabu yako,” alisema kipa huyo wa zamani wa Chelsea katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mechi ya marudiano ya Jumatano.
“Lakini kinachonisumbua ni kuona ushangiliaji wa Vinicius ukitumika dhidi yake. Vini hakufanya jambo lolote baya. Alisherehekea kwa namna ile ile ambayo wapinzani wengi wamekuwa wakisherehekea wanapofunga dhidi yetu.
“Kilichotokea kimetokea na hatuwezi kuhalalisha kitendo kinachoshukiwa kuwa cha kibaguzi kwa sababu ya sherehe. Nafikiri kama jamii tunapaswa kuacha kuwa wajinga.”
Ilifichuka Jumanne kuwa Prestianni alisafiri pamoja na kikosi cha Benfica kwenda Hispania licha ya kutoruhusiwa kucheza katika mechi ya Jumatano usiku.
Mirror Football inaelewa kuwa Prestianni anaweza kufungiwa hadi mechi 10 endapo atapatikana na hatia ya kumbagua Vinicius Jr kwa misingi ya rangi, ingawa Benfica na mchezaji huyo wamesisitiza kuwa hakufanya kosa lolote.