City yabeba FA, bado Premier
Muktasari:
- Semenyo aliendelea kuwa tishio kwa Chelsea na baadaye alipoteza nafasi nyingine nzuri baada ya kumpita Marc Cucurella kabla ya kupiga shuti lililotoka nje.
LONDON, ENGLAND: UBORA wa kiungo mshambuliaji wa Manchester City, Antoine Semenyo umeibeba timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la FA baada ya kuifunga Chelsea bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Wembley.
Ulikuwa ni ushindi muhimu kwa kikosi cha kocha Pep Guardiola ambacho kimebeba tena taji hilo tangu mwaka 2023 licha ya kucheza fainali mbili zilizopita bila mafanikio.
City walianza mchezo kwa kutawala umiliki wa mpira na kutengeneza nafasi za mapema huku Semenyo akipiga mashuti mawili yaliyozuiwa na mabeki wa Chelsea, Omar Marmoush pia alikosa utulivu aliposhindwa kuunganisha vizuri mpira uliotokana na moja ya nafasi hizo.
Licha ya City kuonekana kucheza kwa kujiamini, Chelsea walijaribu kufanya mashambulizi ya kushtukiza kupitia Joao Pedro lakini mshambuliaji huyo alidhibitiwa vizuri na beki Abdukodir Khusanov.
Dakika ya 27, Erling Haaland aliweka mpira wavuni baada ya pasi ya Matheus Nunes lakini bao hilo lilikataliwa kwa madai ya kuotea.
Semenyo aliendelea kuwa tishio kwa Chelsea na baadaye alipoteza nafasi nyingine nzuri baada ya kumpita Marc Cucurella kabla ya kupiga shuti lililotoka nje.
Kipindi cha pili Guardiola alimwingiza Rayan Cherki ambaye alileta mabadiliko makubwa kwenye safu ya ushambuliaji ya City, ndani ya dakika mbili baada ya kuingia, alihusika katika shambulizi lililozaa nafasi kwa Semenyo ambaye kichwa chake kilipaa juu ya lango.
Chelsea walionekana kuongezeka nguvu kadri muda ulivyokwenda huku Moises Caicedo, Wesley Fofana na Reece James wakijaribu kuisukuma timu mbele lakini safu ya ulinzi ya City ilisimama imara.
Dakika ya 72, ndipo Wembley ililipuka kwa furaha upande wa mashabiki wa City baada ya Haaland kutoa pasi ya kurudisha nyuma ambayo ilimaliziwa kwa ustadi mkubwa na Semenyo, mpira ukatinga wavuni karibu na nguzo upande wa kulia mwa Sanchez.
Baada ya bao hilo, Enzo Fernandez alikaribia kusawazisha kwa Chelsea lakini juhudi zake hazikutosha. Sanchez aliendelea kuwaokoa Chelsea kwa kuzuia mashuti ya Matheus Nunes na Cherki huku City wakihakikisha wanatunza ushindi huo hadi mwisho.
Kwa ushindi huo, Manchester City imechukua FA Cup kwa mara ya nane katika historia yao na kufikisha idadi sawa na Chelsea. Aidha, ushindi huo unawapa morali kubwa kuelekea hatua za mwisho za mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.
Kwa upande wa Chelsea, kipigo hicho kinamaanisha wamepoteza fainali ya nne mfululizo za FA, hali inayozidi kuongeza presha ndani ya klabu hiyo.