Chelsea kumtoa Jackson kwa Juve
Muktasari:
- Chelsea wanatafuta mbadala wa Marc Cucurella baada ya beki huyo wa kushoto kuuzwa Real Madrid.
LONDON, England: Chelsea FC huenda wakamtumia mshambuliaji Nicolas Jackson kama sehemu ya makubaliano ya kumsajili beki wa Juventus FC, Andrea Cambiaso.
Chelsea wanatafuta mbadala wa Marc Cucurella baada ya beki huyo wa kushoto kuuzwa Real Madrid.
Hata hivyo, Juventus wameweka bei ya pauni35 milioni kwa Cambiaso, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Italia. Ripoti zinaeleza kuwa Chelsea kwa sasa wako tayari kulipa takribani pauni milioni 25 pekee, kiasi ambacho ni chini ya thamani inayotakiwa na Juventus.
Jackson suluhisho
Jackson, ambaye alitumia msimu uliopita kwa mkopo Bayern Munich, anaweza kuwa njia ya kusaidia pande zote mbili kupata kile wanachotaka.
Juventus wanatafuta mshambuliaji mpya na pia wanawafuatilia Randal Kolo Muani, ambaye alicheza kwa mkopo katika Tottenham Hotspur kutoka Paris Saint-Germain msimu uliopita, pamoja na Alexander Sorloth wa Atletico Madrid.
Hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa Juventus wanamvutiwa sana Jackson mwenye umri wa miaka 25, ambaye kwa sasa yuko katika Kombe la Dunia akiwa na Senegal.
Chelsea wanaweza kujaribu kufanya makubaliano ya kubadilishana wachezaji au kumuuza Jackson kwa Juventus kwa masharti yatakayorahisisha usajili wa Cambiaso.
Barcelona pia wanamfuatilia Cambiaso
FC Barcelona pia wanamuwinda Cambiaso na wanadaiwa kuwa tayari kumjumuisha Ronald Araujo pamoja na fedha katika ofa yao.
Cambiaso mwenye miaka 26 ana uwezo wa kucheza kama beki wa kushoto au winga-beki, jambo linalomfanya kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa sokoni.
Juventus ina ukata
Mambo yanaweza kwenda kwa kasi katika siku zijazo kwa sababu Juventus wanaaminika kuwa chini ya presha ya kukusanya fedha kupitia mauzo ya wachezaji kabla ya mwisho wa Juni ili kukidhi kanuni za kifedha.
Hata hivyo, mustakabali wa Jackson katika Chelsea FC ndio utakaokuwa na mchango mkubwa katika kuamua kama dili hilo litafanyika au la.
Iwapo Chelsea wataamua kwamba Jackson hayupo katika mipango yao ya muda mrefu, basi uwezekano wa kumuona akihamia Juventus na Cambiaso kuelekea Stamford Bridge unaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.