Carrick awaonya mastaa kuhusu UEFA
Muktasari:
- United ambayo jana ilikuwa nyumbani Old Trafford kumenyana na Aston Villa ambayo imelingana nayo pointi zote zikiwa na 51, inakamata nafasi ya tatu na kuwa miongoni mwa timu zinazopewa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
MACHESTER, ENGLAND: KOCHA wa mpito wa Manchester United, Michael Carrick amewaonya mapema mastaa wake wasitegemee nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England inatosha kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
United ambayo jana ilikuwa nyumbani Old Trafford kumenyana na Aston Villa ambayo imelingana nayo pointi zote zikiwa na 51, inakamata nafasi ya tatu na kuwa miongoni mwa timu zinazopewa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
“Tunahitaji kila kitu tulicho nacho kuwekeza kikamilifu. Hatuwezi kudhani nafasi ya tano itatosha. Lazima tuwe na malengo makubwa na kushindana vya kutosha katika kila mchezo.”
Kocha huyo, 44, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia kila mchezo; “Tunaangalia kile tunachoweza kufanikisha na kujaribu kupanda kwenye msimamo. Ni mtazamo bora kuliko kudhani tutamaliza wapi.”
Carrick aliweka wazi kikosi chake ni kizuri endapo kitafanya mambo sahihi na anaamini bado wana wachezaji bora wanaoweza kuhakikisha wanatimiza kile ambacho wanakihitaji.
“Timu ni nzuri tunapofanya mambo sahihi na tuna wachezaji wazuri. Tumethibitisha hivi karibuni na tunapaswa kuendelea kuthibitisha.”
Katika vita ya kumaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, Manchester United inakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Aston Villa ambao walicheza nao jana, Chelsea na Liverpool.