Carrick anajua hawezi kupata zali la Solskjaer
Muktasari:
- Carrick aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa muda hadi mwisho wa msimu mwezi uliopita na tayari amepata ushindi mara tatu katika mechi tatu.
MANCHESTER, ENGLAND: MICHAEL Carrick anasisitiza kuwa Manchester United haitafanya mabadiliko ya ghafla au ya pupa kuhusu nafasi yake kama kocha mkuu, kama ilivyofanya hapo awali kwa Ole Gunnar Solskjaer.
Carrick aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa muda hadi mwisho wa msimu mwezi uliopita na tayari amepata ushindi mara tatu katika mechi tatu.
Iwapo Man United itakuwa imeifunga Tottenham nyumbani Jumamosi, itakuwa mara ya kwanza tangu Februari 2024 kushinda mechi nne mfululizo za Ligi Kuu England.
Solskjaer aliteuliwa kuwa kocha wa muda Desemba 2018 na Man United ilianza kipindi chake kwa mfululizo wa ushindi wa kushangaza wa mechi nane. Man United ilishinda mechi 14 kati ya 19 wakati wa kipindi cha Solskjaer kama kocha wa muda kabla ya kuteuliwa rasmi kuwa kocha wa kudumu Machi 2019. Baada ya hapo, Man United ilishinda mechi mbili pekee kati ya mechi zao kumi za mwisho na walipoteza mara sita, hali iliyosababisha kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mkurugenzi wa soka wa Man United, Jason Wilcox, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu, Omar Berrada, wako katika mchakato wa kumtambua kocha mkuu wa kudumu wa klabu kwa msimu ujao.
Carrick anasisitiza kuwa klabu haitabadili mipango yake na kwamba kungekuwa na tatizo iwapo wangefanya hivyo kabla msimu kumalizika Mei 24, aliposema: “Hakuna kilichobadilika, hapana. Kwa kweli, haitabadilisha ninachofanya wala ninavyojisikia kuhusu jambo hili. Ninatambua kikamilifu nafasi niliyopo na wajibu niliyonayo hapa. Tunataka kufanikiwa. Nataka klabu ifanikiwe hata baada ya msimu kumalizika, iwe ni mimi au mtu mwingine. Kwa wakati huu, siwezi kudhibiti hilo na tutaona kitakachotokea. Lakini lengo ni kuboresha timu na kuifanya Man United kuwa imara zaidi na kuendelea kuboreshwa muda wote.”