Carra: Gyokeres? Benchi lingemhusu
Muktasari:
- Arsenal itakwenda Anfield kukabiliana na Liverpool ikiwa ni kipute cha mapema kabisa cha mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England huku ikiwa haina huduma ya staa wake, Havertz.
LONDON, ENGLAND: GWIJI wa Ligi Kuu England na beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher anaamini kocha wa Arsenal, Mikel Arteta angemweka benchi straika Viktor Gyokeres kwenye kipute cha leo Jumapili huko Anfield endapo kama Kai Havertz angekuwa fiti.
Arsenal itakwenda Anfield kukabiliana na Liverpool ikiwa ni kipute cha mapema kabisa cha mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England huku ikiwa haina huduma ya staa wake, Havertz.
Mjerumani huyo amefanyiwa upasuaji wa goti na ikiwa haifahamiki atakuwa nje ya uwanja kwa muda gani, fowadi huyo atakosa mechi muhimu ya leo Jumapili.
Na sasa straika Gyokeres atabeba matumaini makubwa ya mashabiki wa Arsenal katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, ambapo pia itamkosa Bukayo Saka huku pia kukiwa na wasiwasi mkubwa wa kutokuwa na huduma ya nahodha, Martin Odegaard kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya bega.
Gyokeres alijiunga na Arsenal kwa ada ya Pauni 63.7 milioni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na huko anakotoka Sporting Lisbon alifunga mabao 54 katika mechi 52 alizocheza msimu uliopita. Tayari ameshafunga mara mbili kwenye Ligi Kuu England msimu huu, alipofanya hivyo kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Leeds United wikiendi iliyopita, lakini Carragher bado hajashawishika na uwezo wa straika huyo mwenye umri wa miaka 27.
Alipozungumza baada ya Arsenal kuichapa 1-0 Manchester United kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu England msimu huu, Carragher alitoa maoni yake juu ya Arteta kwamba atakuwa akimweka benchi Gyokeres kwenye mechi zote kubwa.
Hilo linatokana na imani yake kwamba Havertz ni mchezaji mzoefu na anayefiti vyema kwenye mfumo wake.
“Naamini Kai Havertz angechaguliwa kuanza mbele ya Gyokeres Jumapili kama asingekuwa majeruhi,” alisema Carragher.