BURGER ZILIMPONZA ANDERSON

LONDON, ENGLAND. NYOTA wa zamani wa Manchester United, Rafael anaamini kwamba aliyekuwa mchezaji mwenzake wa mashetani wekundu wa Old Trafford, Anderson angekuwa bora Dunia lakini aliponzwa na tabia yake ya kupenda kula hovyo burger.
Anderson alijiunga na Manchester United. 2007 akitokea FC Porto ya Ureno akiwa mmoja kati ya wachezaji ambao walikuwa wakionekana kuwa anaweza kufanya makubwa.
Kiungo huyo alijikuta akicheza fainali moja tu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, 2008 akiwa na Manchester United dhidi ya Chelsea kabla ya taratibu kuanza kuongezeka uzito.
Rafael, ambaye kwa sasa anaichezea Istanbul Basaksehir alisema, "Tatizo ni kwamba alikuwa akiumia mara kwa mara na kingine chakula ambacho alikuwa akipenda kula, kiwango chake kiliathirika."

Aliendelea kumuongelea Mbrazil mwenzake kwa kusema, "Alikuwa akionyesha kiwango kikubwa sana akiwa kwenye ubora wake, nadhani angekuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa Duniani."
Licha ya kwamba Anderson alikipiga Old Trafford kwa miaka saba na miezi kadhaa, aliondoka jijini Manchester akiwa mchezaji wa kawaida tofauti na vile ambavyo alikuwa akitazamiwa na kujikuta akirejea nyumbani kwao, Brazil kwa kujiunga na Internacional.