Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bosi Nottingham azichapa na mpwa wa Waziri Mkuu

Muktasari:

  • Mfanyabiashara huyo bilionea mwenye umri wa miaka 58, ambaye pia anamiliki Olympiacos alionekana akiwa na shati lililochanika baada ya vurugu kuzuka katika eneo la wageni maalumu (VIP) wakati wa mchezo huo. Olympiacos iliishinda Real Madrid kwa pointi 92-85 na kutwaa taji  la nne la EuroLeague.

ATHENS, UGIRIKI: BOSI kubwa mmiliki wa Nottingham Forest, Evangelos Marinakis, ameripotiwa kuhusika katika ugomvi uliotokea kwenye mchezo wa fainali ya Ligi ya Kikapu Ulaya (EuroLeague), kati ya Olympiacos na Real Madrid Baloncesto kwenye Uwanja wa Telekom Centre mjini Athens, Ugiriki.

Mfanyabiashara huyo bilionea mwenye umri wa miaka 58, ambaye pia anamiliki Olympiacos alionekana akiwa na shati lililochanika baada ya vurugu kuzuka katika eneo la wageni maalumu (VIP) wakati wa mchezo huo. Olympiacos iliishinda Real Madrid kwa pointi 92-85 na kutwaa taji  la nne la EuroLeague.

Video za CCTV zilizosambaa mirandaoni zinamuonyesha Marinakis akishuka ngazi za eneo la VIP kabla ya kumkabili na kudaiwa kumpiga kibao Grigoris Dimitriadis, ambaye ni mpwa wa Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis. Tukio hilo lilisababisha vurugu kubwa, huku video nyingine zikimuonyesha Marinakis akizuiwa na walinzi pamoja na vizuizi vya usalama akionekana kupaza sauti kwa hasira.

Ripoti za ndani nchini Ugiriki zimeeleza kuwa ugomvi huo unatokana na mvutano wa muda mrefu kati ya makundi yenye ushawishi katika siasa na michezo, ambapo chanzo kinatajwa kurejea mwaka 2022 wakati Ugiriki ilipokumbwa na kashfa iliyojulikana kama Watergate.

Katika sakata hilo, programu ya udukuzi iitwayo “predator” ilidaiwa kutumika kuwafuatilia watu 87, wakiwemo mawaziri wa serikali, viongozi wa jeshi na waandishi wa habari. Dimitriadis alijiuzulu nafasi yake kama katibu mkuu katika ofisi ya Waziri Mkuu baada ya sakata hilo, ingawa maofisa wa serikali walisisitiza kuwa kujiuzulu kwake hakukuhusiana moja kwa moja na kashfa hiyo.

Mwezi Februari mwaka huu, watu wanne walifungwa jela kuhusiana na sakata hilo la udukuzi, lakini hakuna ofisa wa serikali, akiwemo Dimitriadis, aliyefikishwa mahakamani. Marinakis pia anamiliki vyombo kadhaa vikubwa vya habari nchini Ugiriki, ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kuripoti na kuchunguza sakata hilo la udukuzi.

Mbali na mafanikio ya timu ya mpira wa kikapu ya Olympiacos, Marinakis pia ameiongoza Olympiacos kushinda mataji 11 ya Ligi Kuu ya soka nchini humo tangu alipochukua umiliki 2010. Klabu hiyo pia ilitwaa taji la Europa Conference League 2024.

Katika soka la England, Marinakis alinunua Nottingham Forest 2017 na kusaidia kurejea Ligi Kuu kupitia mechi za mtoano 2022.

Baada ya kubaki katika ligi hiyo, Forest ilifanikiwa kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Ulaya 2025. Kikosi cha Vítor Pereira kilifika hatua ya nusu fainali ya Europa League kabla ya kutolewa na Aston Villa waliokuja kuwa mabingwa wa mashindano hayo msimu huu.

Hata hivyo, msimu mgumu wa Ligi Kuu England uliifanya Forest kubadilisha makocha wanne wa kudumu katika jitihada za kukwepa kushuka daraja. Pereira alichukua nafasi ya Sean Dyche mwezi Februari na kufanikiwa kuiokoa timu hiyo. Nottingham ilimaliza msimu kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Bournemouth kwenye dimba la City Ground, na kumaliza katika nafasi ya 16 ikiwa pointi tano juu ya eneo la kushuka daraja.