Bila ‘VAR’ Arsenal, Chelsea, Liverpool zingeathirika zaidi msimu huu
Muktasari:
- Takwimu mpya zilizotolewa na wataalamu wa takwimu wa ‘AceOdds’ zimefichua msimamo wa ligi hiyo bila ya teknolojia hiyo, huku zikionyesha kuwa kinara wa msimamo wa ligi kwa sasa Arsenal, angekuwa kwenye wakati mgumu zaidi.
LONDON, ENGLAND: MBIO za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL) zingekuwa na taswira tofauti msimu huu endapo kusingekuwa na teknolojia ya usaidizi wa video kwa marefa (VAR).
Takwimu mpya zilizotolewa na wataalamu wa takwimu wa ‘AceOdds’ zimefichua msimamo wa ligi hiyo bila ya teknolojia hiyo, huku zikionyesha kuwa kinara wa msimamo wa ligi kwa sasa Arsenal, angekuwa kwenye wakati mgumu zaidi.
Hii inafuatia ushindi wa hivi karibuni wa Arsenal dhidi ya West Ham, ambapo bao la kusawazisha la West Ham lilikataliwa na VAR dakika za mwisho.
Licha ya kwamba vijana wa Mikel Arteta wangeendelea kushikilia usukani wa ligi hata bila VAR, pengo lao dhidi ya wanaofuata lingepungua kwa kiasi kikubwa sana. Badala ya kuongoza kwa tofauti ya pointi tano kama ilivyo sasa, Arsenal ingekuwa mbele kwa pointi moja tu dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City.
Hali hiyo ingempa Pep Guardiola na kikosi chake faida kubwa, kwani wangekuwa na uwezo wa kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili iwapo wangepata ushindi kwenye mchezo wao wa kiporo, huku zikiwa zimesalia mechi mbili tu msimu kumalizika.
Mabadiliko makubwa zaidi yangeonekana kwenye mbio za kuwania nafasi nne za juu ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League). Wakati Manchester United ikisalia thabiti katika nafasi ya tatu na pointi zake 65, klabu ya Brighton ingeshangaza wengi kwa kuruka kutoka nafasi ya saba hadi nafasi ya nne, huku ikiongeza pointi saba na nafasi tatu juu.
Brighton ingeungana na Bournemouth, iliyopanda kwa nafasi moja na alama tano, kuchukua nafasi za Aston Villa na Liverpool ambazo zimeshuka chini kutokana na kufaidika sana na uamuzi wa VAR msimu huu. Liverpool ingeporomoka kutoka nafasi ya nne hadi ya saba katika msimamo huo wa kufikirika.
Katika maeneo ya katikati ya msimamo wa ligi, Everton na Fulham zingepata ahueni kubwa kwa kupanda juu kwa nafasi mbili kila mmoja na kushika nafasi ya nane na tisa. Everton inatajwa kuwa timu ambayo haikupata uamuzi hata mmoja wa VAR uliogeuza matokeo kwa faida yao msimu mzima.
Kwa upande mwingine, Chelsea ingeporomoka hadi nafasi ya kumi baada ya kupoteza nafasi moja, huku takwimu zikionyesha ndiyo timu iliyonufaika zaidi na teknolojia hiyo baada ya kupata faida hiyo mara tisa. Brentford nayo ingepoteza pointi tano na kushuka chini kwa nafasi tatu bila uwepo wa VAR.