Basi la Barca lashambuliwa London
Muktasari:
- Wafanyakazi walilazimika kutengeneza dirisha lililovunjika ili wachezaji waweze kusafirishwa haraka kwenda Uwanja wa Ndege wa Gatwick mara baada ya mechi.
LONDON, ENGLAND: BASI rasmi lililokuwa limebeba timu ya Barcelona lilishambuliwa usiku wa juzi jijini London wakati likienda kwenye Uwanja wa Stamford Bridge kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Chelsea.
Wafanyakazi walilazimika kutengeneza dirisha lililovunjika ili wachezaji waweze kusafirishwa haraka kwenda Uwanja wa Ndege wa Gatwick mara baada ya mechi.
Polisi jijini London wameeleza kwamba tayari wameshaanza kufanya uchunguzi ili kubaini waliohusika na tukio hilo.
Baadhi ya mashabiki wa Barca wanaamini tukio hilo lilikuwa sababu mojawapo iliyochangia timu yao kupoteza utulivu na mwisho kuambulia kichapo cha mabao 3-0.
Hata hivyo kwa benchi la ufundi la Barca mtazamo wao ulikuwa tofauti na kocha Hansk Flick alipoulizwa alisema: "Tunahitaji kuwa na nguvu zaidi, hasa matukio ya kuwania mpira mmoja kwa mmoja, ukiwaangalia Chelsea, wao daima wana nguvu hiyo, wanacheza kwa mwili mmoja, hicho ndicho ninachotaka kuona kutoka kwenye timu yangu. Kuna muda huwa tunaona tunaweza kushinda kwa kumiliki tu mpira, lakini mambo huwa tofauti unapocheza Ligi ya Mabingwa tena dhidi ya timu ambayo inacheza Ligi Kuu England na inashika nafasi ya pili katika msimamo, inabidi utumie nguvu zaidi na kuwa makini muda wote."
"Lakini tulianza vizuri sana mechi, tulikuwa na nafasi kubwa ya kuwa wa kwanza kufunga bao, lakini nafikiri baada ya kadi nyekundu, kila kitu kilibadilika. Haikuwa rahisi kutaka kushinda mechi ukiwa na wachezaji 10, lazima tukubali kipigo hiki na tuangalie mechi zifuatazo."