Baleba kuvunja kibubu Man United
Muktasari:
- Mabosi wa Man United wamewasiliana na wenzao wa Brighton kuulizia uwezekano wa kupata saini ya mkali huyo mwenye umri wa miaka 21 na kinachoelezwa ni kwamba dili hilo lipo hatua za mwisho.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United italazimika kulipa ada itakayovunja rekodi ya uhamisho kama inataka saini ya kiungo wa Brighton, Carlos Baleba kwenye dirisha hili la uhamisho.
Mabosi wa Man United wamewasiliana na wenzao wa Brighton kuulizia uwezekano wa kupata saini ya mkali huyo mwenye umri wa miaka 21 na kinachoelezwa ni kwamba dili hilo lipo hatua za mwisho.
Baleba kwa sasa anathaminishwa kuwa na thamani ya Pauni 76 milioni, lakini Seagulls haina mpango wa kumuuza kwenye dirisha hili na hilo ndilo litakalofanya thamani yake kupanda zaidi.
Na kinachoelezwa Brighton itafikiria mpango wa kumuuza kama ada itakayolipwa itazidi Pauni 115 milioni ambayo iliikubali ilipomuuza Moises Caicedo kwenda Chelsea 2023.
Baleba mkataba wake wa sasa umebakiza miaka mitatu huko Amex Stadium. Kiungo huyo alinaswa na Seagulls kwa ada ya Pauni 23 milioni kutoka Lille miaka miwili iliyopita na sasa anatambulika kama mchezaji mwenye kipaji kikubwa kwenye soka dunia. Man United inamsaka kiungo huyo ili akawe mtu muhimu kwenye mfumo wa kocha Ruben Amorim wa 3-4-3.
Kiungo, Manuel Ugarte aliyenaswa kutoka Paris Saint -Germain kwa ada ya Pauni 50 milioni, Agosti mwaka jana, ameshindwa kuonyesha kiwango cha kuridhisha kwenye pre-season. Na sasa kuna shabiki mmoja wa Man United ameanzisha ukurasa mtandaoni unaofahamika kwa jina la GoFundMe kwa ajili ya kuchangisha pesa za kufanya dili hilo likamilike.
Mapema mwaka huu, mmiliki mwenza wa Man United, bilionea Sir Jim Ratcliffe alisema klabu hiyo ingefilisiuka kama asingetumia mbinu zake za kubana matumzi. Lakini, kwenye dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi, Man United imekuwa moja ya timu zilizofanya matumizi makubwa kwenye Ligi Kuu England.
Imemsajili Ma-theus Cunha kutoka Wolves kwa Pauni 62.5 milioni, Bryan Mbeumo kutoka Brentford kwa Pauni 71 milioni na Diego Leon kutoka Cerro Porteno kwa Pauni 7 milioni na ipo hatua za mwisho kukamilisha dili la Pauni 74 milioni la kumnasa straika Benjamin Sesko kutoka RB Leipzig.