Badala ya AJ, Furry kuzitwanga na huyu
Muktasari:
- Majina kadhaa makubwa yaliwahi kuhusishwa kama wapinzani wake wanaoweza kupigana naye katika pambano lake la kurejea ikiwemo Anthony Joshua, lakini ilishindikana baada ya bondia huyo kupata ajali ya gari Nigeria.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya kupoteza pambano la pili mfululizo dhidi ya Oleksandr Usyk Desemba 2024 na baadae kuamua kustaafu ndondi, Tyson Furry ametangaza atarejea ulingoni mwaka huu ikiwa imepita miezi 14 tangu atoe taarifa hiyo.
Majina kadhaa makubwa yaliwahi kuhusishwa kama wapinzani wake wanaoweza kupigana naye katika pambano lake la kurejea ikiwemo Anthony Joshua, lakini ilishindikana baada ya bondia huyo kupata ajali ya gari Nigeria.
Baada ya tetesi za muda mrefu, pambano la bondia huyu sasa limetangazwa na anatarajiwa kupigana ndani ya miezi mitatu ijayo.
Taarifa kutoka Ring Magazine zinaeleza bingwa huyo wa zamani wa dunia atapambana na Makhmudov katika pambano la uzito wa juu la The Ring, Aprili 11.
Pambano hilo litarushwa mubashara katika Netflix na litafanyika Uingereza na litakuwa pambano la kwanza la bondia huyo kupambana katika ardhi ya nchi yake baada ya takribani miaka minne.
Akizungumza kuelekea pambano hilo, Fury alisema: "Ninafuraha kurejea. Moyo wangu upo katika mchezo huu daima. Kila mtu sasa ajue mfalme amerudi!”
Ukumbi mahsusi wa pambano hilo na mapambano ya awali bado haujatangazwa, lakini imethibitishwa yote yatatangazwa katika wiki chache zijazo.
Makhmudov ni bondia wa uzito wa juu kutoka Urusi anayeishi Canada na ana rekodi ya ushindi mara 21, kati ya hiyo 19 kwa knock-out, na amepoteza mapambano mawili pekee, dhidi ya Agit Kabayel Desemba 2023 na Guido Vianello Agosti 2024.