Asikwambie mtu! Talaka chungu
Muktasari:
- Kocha wa Manchester City, Guardiola na mkewe mrembo Cristina walitaka kulifanya suala hilo la kutalikiana kuwa la kirafiki, lakini sasa mambo yamegeuka, ikitakiwa kukamilika haraka na kutibua uhusiano.
MANCHESTER, ENGLAND: SAKATA la talaka ya Pep Guardiola na mkewe mrembo Cristina Serra limechukua sura mpya huku likitakiwa kumalizwa haraka.
Kocha wa Manchester City, Guardiola na mkewe mrembo Cristina walitaka kulifanya suala hilo la kutalikiana kuwa la kirafiki, lakini sasa mambo yamegeuka, ikitakiwa kukamilika haraka na kutibua uhusiano.
Misukosuko ya ndoa ya Guardiola ilianza kuripotiwa Januari mwaka huu, huku bosi huyo Mhispaniola akiwa kwenye wakati mgumu kibaruani kwake Etihad.
Na sasa kuna hofu kubwa imeibuka kwamba huenda hilo likatibua mwanzo mzuri wa msimu mpya wa Ligi Kuu England kwenye kikosi hicho cha Man City.
Guardiola ameshatangaza kwamba ataachana na miamba hiyo ya Etihad wakati mkataba wake utakapofika ukomo 2027, akidai anataka kujijali mwenyewe.
Taarifa za watu wa karibu na familia hiyo zimefuchua kwamba uhusiano wake na mkewe umebadilika kutoka kwenye urafiki na kuwa uadui, baada ya kuwa na mapishano kidogo kwenye majadiliano ya kuhusu talaka.
Matarajio ni kwamba mchakato wote unaweza kukamilika ndani ya wiki chache na mapema mwezi ujao itatangazwa wawili hao kuachana rasmi.
Waandishi wa habari mashuhuri huko Hispania, Laura Fa na Lorena Vazquez, ambao ndio waliobainisha taarifa hiyo ya kuachana, walisisitiza kwamba ilipofika kwa sasa hakuna namna ya wawili hao kusuluhishwa.
Fa alisema: “Ishu ya kusaini talaka hii itafanyika kwa haraka. Huu ni ushahidi tosha kwamba uhusiano huo umefika kikomo.”
Vazquez alisema: “Uhusiano wao umebadilika kutoka kuwa wa kirafiki hadi uadui. Hatusemi kuna ugomvi mkubwa baina yao, lakini kuachana kwao si kwa kawaida. Wanataka kufanya haraka kumaliza uhusiano wao.”
Pep, 54, na Cristina, 52, wamekuwa pamoja kwa miaka 30, walioana 2014.
Mrembo Cristina, ambaye anajihusisha na biashara zake za mitindo, ameshindwa kuishi Manchester na kuamua kurudi Hispania miaka mitano iliyopita. Na kilichoelezwa wawili hao walikubaliana kuachana Desemba mwaka jana wiki chache baada ya kusaini mkataba mpya Man City.