Arteta ashindwe mwenyewe tu
Muktasari:
- Baada ya miaka sita ya kukinoa kikosi hicho, hatimaye kocha Arteta sasa hatakuwa na kisingizio kingine kutokana na mabosi wake kumletea wachezaji mahiri kabisa wasiopungua wawili wenye viwango bora kwenye kila nafasi.
LONDON, ENGLAND: NDOTO za miaka mingi za Kocha Mikel Arteta zimetimia baada ya Arsenal kumwandalia kikosi chenye wachezaji wawili wenye viwango bora kwenye kila nafasi, kazi anayo.
Baada ya miaka sita ya kukinoa kikosi hicho, hatimaye kocha Arteta sasa hatakuwa na kisingizio kingine kutokana na mabosi wake kumletea wachezaji mahiri kabisa wasiopungua wawili wenye viwango bora kwenye kila nafasi.
Kilichobaki kwa Arteta ni kuipa Arsenal taji la Ligi Kuu England ambalo mara ya mwisho ililinyakua mwaka 2004, huku misimu mitatu iliyopita ikimaliza kwenye nafasi ya pili mfululizo.
Ujio wa Eberechi Eze kwenye kikosi hicho kwa ada ya Pauni 68 milioni akitokea Crystal Palace kinaifanya Arsenal kutumia zaidi ya Pauni 250 milioni kwenye usajili wa dirisha hili la majira ya kiangazi, huku kocha Arteta akifikisha matumizi ya Pauni 1 bilioni tangu alipoanza kuinoa timu hiyo, Desemba 2019.
Kwenye kikosi chake, Arteta amepewa wachezaji wa maana kabisa na kipa namba mbili anayemsaidia David Raya ni Kepa Arrizabalaga, huku ikiwa na beki matata kabisa Cristhian Mosquera, viungo mahiri Christian Norgaard na Martin Zubimendi, winga Noni Madueke, straika Viktor Gyokeres na kiraka Eze.
Jambo hilo linakifanya kikosi cha Arsenal kuwa kipana na kufanya kuwa na walau wachezaji wawili wenye viwango bora kwenye kila nafasi uwanjani.
Mastaa hao wapya wanakuja kuongeza nguvu kwa kuungana na waliokuwapo kwenye kikosi ikiwamo Gabriel, William Saliba, Kai Havertz, Bukayo Saka, Martin Odegaard, Ben White, Gabriel Martinelli, Mikel Merino na Gabriel Jesus kwa kuwataja kwa uchache.