Arteta aanza kutafuta kisingizio
Muktasari:
- Arsenal ilikaribia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England kwa misimu mitatu mfululizo, ilipomaliza nafasi ya pili, mara mbili dhidi ya Manchester City na moja dhidi ya Liverpool.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amekiri majeruhi wengi kwenye kikosi chake limekuwa tatizo linalowatatiza kwenye mchakamchaka wao wa kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England.
Arsenal ilikaribia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England kwa misimu mitatu mfululizo, ilipomaliza nafasi ya pili, mara mbili dhidi ya Manchester City na moja dhidi ya Liverpool.
Lakini, mara zote vita yao ya kushinda ubingwa umekwamishwa kwa mambo mawili, kiwango cha timu kushuka pamoja na majeruhi. Na Arteta amekiri jambo hilo linaweza kuwa tatizo tena msimu huu na Arsenal tayari imeshapoteza mastaa kadhaa muhimu kwa kuwa majeruhi.
Kai Havertz na Bukayo Saka watakuwa nje ya uwanja kwa muda, lakini kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield, wakati Arsenal ilipochapwa 1-0, ilimpoteza beki wao wa kati, William Saliba baada ya kuhisi maumivu ya kifundo cha mguu.
Alipozungumza mwisho wa mechi hiyo, Arteta alisema:
“Nimehuzunika sana kwa matokeo. Lakini, najivunia wachezaji wangu. Timu zote mbili zilicheza kwa viwango bora, ilikuwa mechi ya kuamriwa kwa makosa binafsi au viwango vya maajabu.
“Huwezi kutawala mechi dakika zote 90 uwanjani hapa, haiwezekani. Mwisho wa yote, unahitaji kutafuta njia ya kushinda mechi za aina hii. Tulikuwa na kiwango bora msimu uliopita. Tulimpoteza Martin (Odegaard), tumempoteza Kai (Havertz) na kisha tumempoteza Bukayo (Saka). Kwenye kipindi cha kupasha misuli moto, tumempoteza Saliba.”
Arteta alielezea ishu ya Saliba akisema: “Aliteguka enka wakati wa kupasha misuli.
“Aliingia uwanjani na kusema ataendelea kucheza, lakini baada ya muda mfupi tu, alishindwa kuendelea. Tunashukuru Mungu tunaye Mosquera, ambaye alicheza mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu England, lakini alicheza vizuri sana.”
Arsenal sasa ina mapumziko ya wiki mbili kuhakikisha wachezaji wake wanarudi kwenye viwango bora wakati huu wa mapumziko ya mechi za kimataifa. Mechi ijayo ya Arsenal kwenye Ligi Kuu England wiki mbili zijazo itakipiga na Nottingham Forest uwanjani Emirates.