Kutoka marafiki wa shule hadi wazazi, simulizi ya mapenzi ya Julian Alvarez na Maria
Muktasari:
- Hata hivyo, maisha yake nje ya soka yana simulizi nyingine nzuri hasa uhusiano wake na mpenzi wake wa muda mrefu, Maria Emilia Ferrero, 26, ambaye ni shahidi wa kweli kuhusu jitihada za Alvarez zilizoleta matokeo makubwa tunayoona kwa sasa.
Mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez, 26, ni miongoni mwa mastaa wanaowika katika soka duniani akishinda mataji mengi makubwa akiwa na kikosi cha timu yake ya taifa ya Argentina ambacho kimenza vizuri Kombe la Dunia 2026.
Hata hivyo, maisha yake nje ya soka yana simulizi nyingine nzuri hasa uhusiano wake na mpenzi wake wa muda mrefu, Maria Emilia Ferrero, 26, ambaye ni shahidi wa kweli kuhusu jitihada za Alvarez zilizoleta matokeo makubwa tunayoona kwa sasa.
Moja ya vitu vinavyovutia zaidi kuhusu uhusiano wa Alvarez na Emilia ni historia yao ndefu, walikuwa marafiki tangu shuleni na waliendelea kuwa karibu hata baada ya mchezaji huyo kuhamia England akijiunga na Manchester City alipocheza hadi mwaka 2024.
Uhusiano wao ulionekana zaidi katika Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar ambapo Emilia alionekana mara nyingi kwenye majukwaa akimshangilia Alvarez. Baada ya Argentina kutwaa kombe hilo, wawili hao walisherehekea pamoja uwanjani ushindi huo, na picha zao zilisambaa mitandaoni.
Hata hivyo, baada ya Alvarez kufunga mabao manne kwenye michuano hiyo, shabiki mmoja aliripotiwa kuanzisha ombi kwenye tovuti ya Change.org akitaka wawili hao waachane. Tukio hilo lilitokea baada ya Emilia kudaiwa kumzuia Alvarez kupiga picha na mashabiki.
Inasemekana Emilia alisikika akisema: Jamani, pigeni picha moja tu halafu tunaondoka. Ila licha ya tukio hilo, wawili hao bado wameonekana kuwa na uhusiano imara na wanaendelea kuwa pamoja hadi sasa.
Emilia ambaye ni mkufunzi wa mazoezi ya viungo, alizaliwa huko Calchin, Argentina mnamo Juni 13, 2000, hivyo amezidiwa takribani miezi minne na Alvarez ambaye alizaliwa Januari 31, 2000. Inaripotiwa kuwa alisoma shule moja ya sekondari, hivyo inaaminika kuwa wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza shuleni hapo.
Kwa hiyo kabla ya uhusiano rasmi, ukaribu wao umekuwepo kwa miaka mingi, tangu kipindi Alvarez hajulikani hadi sasa anapotambulika kwa uwezo wake wa kufunga magoli ya viwango.
Taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa wawili hao wamekuwa kwenye uhusiano rasmi kwa zaidi ya miaka saba sasa. Kwa kuwa walikulia eneo moja na kusoma shule moja, walijenga ukaribu tangu wakiwa vijana wadogo.
Kwa sasa Emilia ni mtu maarufu kwenye mitandao ya kijamii akiwa na wafuasi (followers) zaidi ya 695,000 kwenye Instagram. Mara nyingi huonekana akiposti maudhui yanayohusiana na ushirikiano wake na kampuni kama Alo Yoga pamoja na chapa nyingine.
Hata hivyo, hapendi kusaka umaarufu kupitia jina la mpenzi wake huyo, jambo ambalo ni tofauti kabisa na wapenzi wengi wa mastaa wakubwa duniani. Yeye anapenda kufanya mambo yake nyuma ya pazia na kuishi maisha yenye usiri kiasi, hivyo si mtu wa kuweka kila kitu mtandaoni.
Kufikia Juni 2025, wawili hao walitangaza kwamba walikuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza ambaye ni mvulana. Mtoto huyo alikuja kuzaliwa mwanzoni mwa Januari 2026, ambapo alipewa jina la Amadeo.
Ingawa bado hawajafunga ndoa, kwa sasa wawili hao wanaendelea kujenga familia yao pamoja licha ya majukumu makubwa ya uwanjani yanayomkabili Alvarez.
Juni 13, ilikuwa ni birthday ya Emilia akisheherekea kutimiza umri wa miaka 26, kipenzi chake Alvarez kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 19.7 alimwandikia ujumbe ufuatao.
"Umekuwa rafiki bora zaidi, mama bora zaidi na mtu yuleyule wa kipekee niliyempenda. Asante kwa upendo mwingi, uvumilivu wako na kwa kufanya maisha yetu yawe bora kila siku. Heri ya kuzaliwa mpenzi wangu, tunakupenda,” alieleza Alvarez.
Ingawa presha ya kucheza soka katika kiwango cha juu inaweza kuwa kubwa, lakini Alvarez anaonekana kuwa na furaha zaidi akiwa na familia na yake. Kuanzia mwanzo wake wa maisha ya soka akiwa River Plate hadi mafanikio barani Ulaya, Emilia ndiye amekuwa mtu wake wa karibu zaidi akimpa sapoti.
Kwa miaka mingapi Emilia amehudhuria mechi nyingi za Alvarez kuanzia EPL, La Liga, Copa America na Kombe la Dunia la Qatar lakini awamu hii ameshindwa kwenda kutokana mtoto wao bado ni mchanga.
Ikumbukwe kikosi cha Argentina kimewasili kwenye Kombe la Dunia 2026 kikiwa na mastaa wenye majina makubwa ambao pia wameongozana na wapenzi wao. Mmoja wao ni Lionel Messi na mkewe Antonela Roccuzzo ambaye walifunga ndoa mwaka 2017.
Mke wa Messi ambaye amepewa jina la First Lady wa soka, amekuwa pamoja na mshindi huyo wa Ballon d’Or tangu walipokuwa watoto huko Rosario, kabla ya mafanikio yake makubwa akiwa na FC Barcelona, kisha Paris Saint Germain (PSG), na sasa Inter Miami.