Arsenal, Liverpool ‘big no’ kwa Alvarez

Muktasari:
- Alvarez mwenye umri wa miaka 25, alifurahia msimu wa kwanza wa mafanikio na vigogo hao wa Hispania, akifunga mabao 29 katika michuano yote baada ya kuhamia La Liga akitokea Manchester City kwa Pauni 80 milioni.
MADRID, HISPANIA: MABOSI wa Atletico Madrid wameeleza kuwa straika wa timu hiyo, Julian Alvarez ataendelea kusalia kuwa mchezaji wao msimu ujao licha ya timu kadhaa za Ligi Kuu England kutaka kumsajili.
Alvarez mwenye umri wa miaka 25, alifurahia msimu wa kwanza wa mafanikio na vigogo hao wa Hispania, akifunga mabao 29 katika michuano yote baada ya kuhamia La Liga akitokea Manchester City kwa Pauni 80 milioni.
Staa huyo wa kimataifa wa Argentina alionekana kuwa na kiwango bora alipokuwa Man City licha ya kushindania nafasi na Erling Haaland.
Arsenal na Liverpool ndizo klabu zilizohusishwa na Alvarez kabla ya dirisha hili la usajili kufunguliwa ikiwa ni katika harakati za kuboresha safu za ushambuliaji.
Hata hivyo, rais wa Atletico, Enrique Cerezo amesema hawana mpango wa kumuuza licha ya kupokea ofa kubwa.
“Julian Alvarez ni mchezaji wa Atletico Madrid na atasalia kuwa mchezaji wa Atletico Madrid,” Cerezo ameliambia gazeti la Marca juzi, usiku.
Bado haijajulikana kama Arsenal au Liverpool zitajaribu kuwasilisha ofa Atletico kwa ajili ya staa huyo.
Gazeti hilo hilo liliripoti mwezi uliopita kuwa Arsenal ilikuwa inaongoza harakati za kumsajili Alvarez.
Pia iliripotiwa kwamba Alvarez mwenyewe alikuwa anasita kuhusu kurejea England, licha ya mafanikio akiwa Man City ambapo kuondoka kwake kuliwagawa mashabiki. Iwapo Alvarez itashindikana kumpata, Arsenal inatarajiwa kuelekeza juhudi kwa Viktor Gyokeres na Benjamin Sesko. Kwa Liverpool inhusishwa na Hugo Ekitike.