Ander Herrera amtaka Neymar Man United

PARIS, HISPANIA. KIPENZI cha muda wote cha mashabiki wa Manchester United, Ander Herrera amewaambia mabosi wa klabu hiyo ya Old Trafford kile ambacho timu itavuna endapo watafanya mchakato na kukamilisha dili la kumsajili supastaa, Neymar.

Ripoti kutoka Ufaransa zimekuwa zikihusisha Man United na mpango wa kumsajili supastaa wa kimataifa wa Brazil, Neymar kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku mwanasoka huyo ghali duniani - akidaiwa kuwa na mpango wa kuhama Parc des Princes.

Neymar alijiunga na Paris Saint-Germain kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia, Pauni 198 milioni mwaka 2017 - lakini tayari anaonekana kujiandaa kuachana na klabu hiyo ya Ligue 1 baada ya mashabiki wa timu hiyo ya Paris kumfuata nyumbani kwake na kumtaka aondoke.
Herrera kwa misimu mitatu amecheza timu moja na Neymar na kushiriki pamoja vyumba vya kubadilishia nguo kabla ya kwenda kujiunga na Athletic Bilbao kwa mkopo katka dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana na kisha kunaswa jumla dirisha la Januari mwaka huu.

Kiungo huyo wa Kihispaniola, Herrera, ambaye alikuwa mchezaji wa Man United kwa miaka mitano, alisema Neymar ni mmoja wa wachezaji bora duniani na amethibitisha hilo wakati walipokuwa pamoja Ufaransa.
"Neymar ni mmoja kati ya wachezaji watano bora duniani na mshindani kwenye Ballon d'Or sambamba na (Kylian) Mbappe," alisema Herrera mwaka 2019. Alisema maneno hayo katika mkesha wa mechi yake ya kwanza ya Ligue 1, ambayo ilimalizika kwa PSG kushinda 1-0 dhidi ya Strasbourg, mchezo ambao Neymar - ndiye aliyefunga bao la ushindi dakika za mwisho.

"Nimepagawa na nina furaha kwa kucheza na Neymar," aliongeza. "PSG ni fursa adimu kwangu kwa maana ya kuja kucheza timu moja na wachezaji kama Neymar, Kylian Mbappe au Marco Verratti."
Miaka mitatu baadaye, hakuna Ballon d'Or kwa Neymar, lakini hilo limemfanya hata Herrera ashangazwe, aliposema: "Nilidhani alishachukua Ballon d'Or tayari, lakini siwezi kusema haiwezekani. Ilikuwa furaha kwangu kuwa naye timu moja," alisema Herrera alipozungumza na AS mwaka 2022. Kwa kauli hizo za Herrera kuhusu Neymar, bila ya shaka atagonga kifute cha 'like' kwenye posti yoyote itakayowahusu Man United kumtaka Mbrazili huyo itakayowekwa kwenye mitandao ya kijamii. Na kwa kauli ya Herrera, kama atafuatwa na mabosi wa Man United na kuulizwa kuhusu Neymar, hakuna shaka jibu lake litakuwa moja tu "mchukueni".

Man United inahitaji kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, ambapo mshambuliaji Wout Weghorst atarudi kwenye klabu yake ya Burnley muda wake wa mkopo utakapokwisha mwisho wa msimu huku ikiwa haieleweki kuhusu Anthony Martial. Martial alionyesha vitendo vilivyoibua maswali mengi alipotolewa dhidi ya Bournemouth Jumamosi iliyopita, licha ya Kocha Erik ten Hag kuamua kulipuuzia jambo hilo, aliposema: "Nadhani amecheza vizuri, amerudi kutoka kwenye benchi, yupo sawa."

Man United imehusishwa na majina kibao ya mastraika, ikiwano nahodha wa England, Harry Kane na straika wa Atalanta, Rasmus Hojlund. Mkali wa Napoli, Mnigeria Victor Osimhen naye ametajwa kuwamo kwenye rada ya Ten Hag baada ya chama hilo la Old Trafford kurejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Man United bado hawajajihakikishia nafasi kwenye Top Four, lakini watahitaji pointi moja tu katika mechi zao mbili zijazo dhidi ya Chelsea na Fulham ili kuungana na Manchester City, Arsenal na Newcastle United kwenye timu zitakazowakilisha Ligi Kuu England kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Man United endapo itashinda mechi zake zilizobaki, itamaliza msimu kwenye nafasi ya tatu.

Newcastle, ambao pia wamekuwa wakihusishwa na Neymar, wao wameshakata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya Leicester City usiku wa juzi Jumatatu. PSG nao watarejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, hasa wakiwa mabingwa wa Ligue 1 na hilo litatimia kama wataibuka na ushindi dhidi ya Auxerre, Jumapili.