Ancelotti atoa msimamo Real Madrid

Muktasari:
- Tangu kuanza kwa msimu huu, Ancelotti amekuwa akidaiwa kukalia kuti kavu kutokana na kiwango cha kutoridhisha kilichoonyeshwa na Madrid na Xabi Alonso ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa Bayer Leverkusen ndio anapewa nafasi kubwa ya kupewa mikoba.
MADRID, HISPANIA: KOCHA wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema kuwa hana uhakika juu ya hatma yake na kusisitiza kwamba ataondoka ikiwa mkataba wake utavunjwa.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Ancelotti amekuwa akidaiwa kukalia kuti kavu kutokana na kiwango cha kutoridhisha kilichoonyeshwa na Madrid na Xabi Alonso ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa Bayer Leverkusen ndio anapewa nafasi kubwa ya kupewa mikoba.
Mkataba wa sasa wa Ancelotti ambaye amesema hana mpango wa kujiuzuru unatarajiwa kumalizika mwaka 2026 sawa na ule wa Alonso ambaye Mkurugenzi mtendaji wa Leverkusen amesisitiza kuwa ana matumaini makubwa ya kuona anabakia kuifundisha timu hiyo.
"Sijui ni lini(ataondoka), Sitaki mimi ndio niamue. Jambo pekee nililo wazi ni kwamba sidhani kama nitajiuzulu wakati wowote, rais ndie atakayefanya hivyo. inaweza ikatokea tu huenda mapema au ikachelewa."
Januari mwaka huu. Ancelotti alikanusha uvumi wa kwamba alikubaliana na mabosi wa timu hiyo kuondoka mwishoni mwa msimu bila kujali matokeo."
"Nataka kuwa wazi sana: tarehe ya kuondoka kwa klabu hii haitawahi kuamuliwa na mimi katika maisha yangu," alisema.
Ancelotti alisaini mkataba mpya kama kocha mkuu wa Madrid mwishoni mwa 2023, akithibitisha kuendelea kuifundisha hadi 2026, na inaonekana hana haraka ya kuchukua changamoto mpya.
Kocha huyu mwenye umri wa miaka 65 ameiongoza timu yake kutwaa mataji 10, ikiwa ni pamoja na mawili ya Ligi ya Mabingwa, tangu alipojiunga tena kwa kipindi cha pili cha uongozi mwaka 2021. Pia yeye ni ndio kocha aliyeshinda mataji mengi zaidi (15) katika historia ya timu hiyo.
Kwa mujibu wa Mail Sport, Mbali ya Alonso, Madrid pia inahusishwa na kocha wa Bournemouth, Andoni Iraola.