Ana kwa ana na Wabrazili wa Chelsea wanaogandana muda wote
Muktasari:
- WAKIWA wamekusanyika katika sehemu ya chini ya mgahawa wa Kibrazili, Kaskazini-Magharibi mwa London, wapo ndugu watatu wa Chelsea ambao ni mara chache sana hutengana.
LONDON, ENGLAND: WAKIWA wamekusanyika katika sehemu ya chini ya mgahawa wa Kibrazili, Kaskazini-Magharibi mwa London, wapo ndugu watatu wa Chelsea ambao ni mara chache sana hutengana.
Ni wazi kuwa kiongozi wao ni Joao Pedro anapoketi kwa mahojiano, katika mgahawa anaoupenda tangu alipojiunga na Watford akiwa kijana.
Pembeni yake wapo wachezaji wenzake wa Chelsea na raia wenzake wa Brazil, Andrey Santos (21) na Estevao Willian (18).
Pedro, mwenye miaka 24, anawatia moyo wenzake wazungumze zaidi huku akimsaidia kinda huyo nyota katika mahojiano yake ya kwanza na moja ya gazeti maarufu la Uingereza.
Estevao anaonekana mwenye kujiamini uwanjani, lakini nje ya uwanja ni mwenye aibu hadi anapopewa bakuli la coxinha (vitumbua vya kuku vilivyokaangwa na jibini ndani). Baada ya hapo, mazungumzo yanachangamka huku watatu hao wakitaniana na kuchekana, licha ya Estevao bado kuwategemea marafiki zake wawili kumsaidia kutafsiri anapoendelea kujifunza Kiingereza.
Mambo yanaonekana kwenda vizuri kwani walipoulizwa jinsi wanavyoweza kuelezeana, wote walijibu kwa neno moja: “Ndugu.”
Nyota hao watatu wa Samba wanatarajia kumaliza msimu kwa kishindo na pia kushiriki fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico katika kipindi cha majira yajayo ya kiangazi.
Mahojiano yalikuwa hivi;
Swali: Kila mtu Chelsea anasema hamtengani. Ninyi ni marafiki wakubwa, sivyo?
Joao Pedro: Uhusiano wetu unaendelea kukua. Tunacheza hapa Chelsea na pia katika timu ya taifa. Tunasafiri pamoja na kufanya mazoezi pamoja. Natumia muda mwingi zaidi na wao kuliko hata familia yangu.
Andrey Santos: Ni kweli!
Pedro: Tuko karibu sana mazoezini na hata nje ya uwanja tunajaribu kufanya mambo pamoja. Kwa sababu sisi ni Wabrazili, tumekuja hapa kwa lengo moja.
Santos: Uhusiano huu ni muhimu sana kwetu. Joao ndiye kaka mkubwa!
Estevao Willian: Tunatumia muda mwingi pamoja. Nawapenda!
Kwangu kuzoea maisha hapa ilikuwa rahisi kwa sababu walinisaidia kila siku.
Swali: Kutoka Brazil hadi London ni safari ndefu kwa kijana mdogo. Umeonaje maisha hapa?
Estevao: Kitu kizuri kuhusu London ni kwamba nilikuwa naishi Sao Paulo, na kuna mfanano fulani ni jiji kubwa na lenye shughuli nyingi. Kitu kibaya ni hali ya hewa, nahisi baridi sana!
Pedro: Ataizoea! Mimi napenda London. Nimejifunza mambo mengi hapa, aina tofauti za vyakula, Kihispania, Kiingereza.
Santos: Na sasa Kifaransa! Pedro: Ndiyo, najaribu pia kujifunza Kifaransa. Utamaduni wa hapa umenisaidia kukua kwani nilikuja nikiwa mtoto. Ninafurahia kuishi hapa, hasa sasa nikiwa Chelsea. Swali: Joao, ulipoanza Watford uliambiwa ulikuwa na jazba sana uwanjani. Je, umebadilika? Santos: Bado yuko hivyo hivyo!
Pedro: Ndio, bado. Nikikosa hamasa hiyo ni bora niachane na soka. Wachezaji wa Amerika Kusini wako hivyo. Kama Moises Caicedo na Enzo Fernandez, sisi tuna moto ndani. Kila mmoja anataka kushinda.
Swali: Estevao, mashabiki wameanza kukuimba haraka sana. Wanakuita pia “Steve”. Unalionaje hilo?
Estevao: Siwezi kuamini! Lakini sijali wananiita nini. Nafurahia jinsi wanavyoimba. Pedro: Nilipokuja England watu hawakuweza kutamka jina langu vizuri. Waliniita John!
Swali: Kocha Liam Rosenior amekuwa na mchango mkubwa kwenu? Pedro (akitania): Baba yake, baba yake!
Santos: Tangu alipokuja imekuwa rahisi kwangu kwa sababu tayari nilishafanya naye kazi. Tunafahamiana vizuri sana na nina furaha kufanya naye kazi.
Pedro: Yuko wazi sana. Akiona jambo anakwambia moja kwa moja. Wiki ya kwanza tu nilizungumza naye mara nne! Wachezaji wengi wanapenda uwazi huo. Swali: Joao, kocha anasema unaweza kuwa mmoja wa washambuliaji bora duniani. Unaweza?
Pedro: Natumaini!
Santos: Bila shaka anaweza.
Estevao: Hakika! Wewe ni namba 9 wetu!
Pedro: Wenzangu wanaamini kwangu. Najitahidi kila siku. Najua kuna mazungumzo mengi kuhusu mimi sasa, lakini mimi ni yule yule tangu nilipokuja England. Naamini uwezo wangu. Ukifunga na mambo yanaenda vizuri, watu watazungumza, lakini nataka kubaki mnyenyekevu na kufanya kazi yangu.
Swali: Estevao, ni tukio gani limekukaa zaidi ukiwa na jezi ya Chelsea?
Estevao: Liverpool!
Pedro: Kila mtu alifurahia bao lake dhidi ya Liverpool. Ilikuwa wiki zake za kwanza katika mchezo mkubwa. Alipoingia na kufunga bao la mwisho, nilisherehekea kama ni ndugu yangu. Tunahitaji kumpa muda aendelee kufurahia kila hatua.
Swali: Mlishinda taji Marekani majira ya joto yaliyopita katika Kombe la Dunia la Klabu. Mnaonaje kurudi huko kwa Kombe la Dunia na Brazil?
Santos: Ilikuwa ngumu sana majira yaliyopita.
Pedro: Ilikuwa vigumu uwanja ulikuwa kama moto, mechi zilikuwa kali sana na kushindwa kulimaanisha kuondoka mashindanoni. Lakini, tulifurahia na tunatumaini tutashinda tena.
Estevao: Nina wasiwasi kidogo lakini pia nina furaha sana. Ni ndoto yangu kuwa kwenye kikosi cha Brazil.
Pedro: Kwa uhusiano huu tulio nao, naamini tunaweza kushinda angalau taji moja zaidi na Chelsea. Hilo ndilo tunalotaka sisi na mashabiki. Kisha Kombe la Dunia tunatumaini tutakwenda pamoja na kufanya vizuri.