Amorim ataka Sesko, Hojlund wacheze wote
Muktasari:
- Bosi huyo wa benchi la ufundi la Man United ameanza kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na straika wa RB Leipzig juu ya dili la Pauni 70 milioni.
CHICAGO, MAREKANI: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amebainisha kuwa na mpango wake ambao utawahusisha Benjamin Sesko na Rasmus Hojlund.
Bosi huyo wa benchi la ufundi la Man United ameanza kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na straika wa RB Leipzig juu ya dili la Pauni 70 milioni.
Hata hivyo, hilo halina maana ya kwamba litafikisha zama za Hojlund huko Old Trafford kufika mwisho, hasa baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye mechi ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Bournemouth uwanjani Soldier Field.
Kocha Amorim ana uhakika ataweza kurudia mafanikio aliyopata alipokuwa na straika Viktor Gyokeres huko Sporting Lisbon atakapomnasa Sesko aongoze safu ya ushambuliaji Man United.
Kocha huyo wa Man United anamshawishi straika huyo mwenye kimo cha futi 6 na inchi 5 kuwa kwenye viwango bora kabisa chini yake. Sambamba na hilo, kocha Amorim anaamini Sesko atakwenda kuwa mshambuliaji kiongozi wa Man United ambaye ilimkosa kwenye msimu uliopita.
Kocha huyo Mreno anaamini pia uwepo wa Sesko utampandisha kiwango Hojlund na kuwa mmoja wa washambuliaji hatari kabisa uwanjani kutokana na uwepo wa vita ya kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Kuwapo kwa vita ya namba kutamfanya Hojlund kupambana na sio kucheza kwa kuwa na uhakika kwamba anapata tu nafasi kwa sababu hakuna straika mwingine mwenye makali ya kutosha.
Hilo ndilo linalomfanya kocha Amorim kuhitaji kumbakiza Hojlund kwenye klabu kuliko kumfungulia mlango wa kutokea. Hata hivyo, kumsajili Sesko hakuonekani kama kutakuwa mwisho wa matumizi ya Man United kwenye usajili, licha ya kwamba saini ya staa huyo wa Slovenia utawafanya kuvuka matumizi ya Pauni 200 milioni.
Eneo jingine ambalo kocha Amorim anataka kuliboresha ni kumpata kipa wa kuja kushindania namba na Andre Onana, huku kwenye eneo hilo kukiwa na makipa kibao wakihusishwa akiwamo yule wa Antwerp, Senne Lammens.