Aliyemtangaza baba'ke Messi kafariki dunia aacha kazi
Muktasari:
- Pena, alitoa taarifa hiyo wakati wa kipindi cha moja kwa moja cha El Show del Verano, akidai kuwa Jorge Messi (68) amefariki, jambo lililozua mshtuko mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka duniani.
BUENOS AIRES, ARGENTINA: MTANGAZAJI maarufu wa televisheni nchini Argentina, Florencia Pena, ameamua kuacha kazi katika kituo cha Luzu TV baada ya kutangaza kimakosa kifo cha baba wa nahodha wa Argentina, Lionel Messi, Jorge Messi.
Pena, alitoa taarifa hiyo wakati wa kipindi cha moja kwa moja cha El Show del Verano, akidai kuwa Jorge Messi (68) amefariki, jambo lililozua mshtuko mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka duniani.
Taarifa hiyo ilitolewa saa chache baada ya Messi kuiongoza Argentina kuanza kwa kishindo fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Algeria huku nyota huyo wa Inter Miami CF akifunga hat-trick.
Wakati wa matangazo hayo, Pena alisema kuwa machozi ya Messi baada ya kufunga yalitokana na taarifa za kifo cha baba yake na hata kudai kuwa nyota huyo angelazimika kuondoka kambini katikati ya mashindano.
Hata hivyo, familia ya Messi ilitoa taarifa rasmi ikikanusha madai hayo na kueleza kuwa Jorge Messi anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na changamoto za kiafya lakini hali yake inaendelea kuimarika.
"Tunathibitisha kuwa Jorge yuko chini ya uangalizi wa madaktari na anaendelea kupata nafuu. Taarifa zilizosambazwa kuhusu kifo chake si za kweli," ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya familia.
Familia hiyo pia ilikosoa vyombo vya habari na watu waliokuwa wakisambaza taarifa zisizothibitishwa kuhusu afya ya Jorge, wakisisitiza kuwa taarifa sahihi zitakuwa zinatolewa na familia pekee.
Baada ya kashfa hiyo, Pena alitoa taarifa ya kuomba radhi kwa familia ya Messi na mashabiki wote walioathiriwa na habari hiyo ya uongo.
"Ninaomba radhi kwa familia ya Messi kwa maumivu ambayo huenda nimeyasababisha. Nina aibu kubwa kwa kuwa sehemu ya kosa hili," alisema mtangazaji huyo.
Alifafanua kuwa taarifa hiyo aliipokea kutoka kwa timu ya uzalishaji wa kipindi hicho akiwa hewani na akaamini kuwa ilikuwa imethibitishwa kabla ya kuitangaza.
Pamoja na maelezo hayo, Pena alikubali kuwajibika kwa kosa hilo na kutangaza kuachana na kazi yake katika kituo cha runinga cha Luzu.
Kwa upande wake, Luzu TV ilisema kusambaza taarifa nyeti bila uhakiki wa kutosha ni jambo lisilokubalika katika misingi ya taaluma ya habari, hivyo uongozi wa kituo hicho umechukua hatua dhidi ya wahusika wote waliohusika.
Wakati huo huo, Messi alizungumza kuhusu machozi yake baada ya ushindi dhidi ya Algeria, akifichua kuwa yalitokana na matatizo binafsi aliyokuwa akipitia siku za karibuni na si masuala ya soka.
"Nimepitia siku ngumu, lakini wenzangu na watu wote waliokuwa karibu nami walinipa nguvu kubwa ya kuvuka kipindi hicho," alisema.