Alexander Isak hadi atake yeye!

Muktasari:
- Kwa mujibu wa kiungo wa zamani wa Newcastle, Mcamerooni Geremi, ambaye alisisitiza staa huyo wa Sweden hana haja ya kuondoka St James’ Park ili kuboresha kiwango chake ndani ya uwanja.
NEWCASTLE, ENGLAND: LIVERPOOL na Arsenal zitalazimika kumtaka straika Alexander Isak kufanya uamuzi mwenyewe kama anataka kuachana na Newcastle United kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Kwa mujibu wa kiungo wa zamani wa Newcastle, Mcamerooni Geremi, ambaye alisisitiza staa huyo wa Sweden hana haja ya kuondoka St James’ Park ili kuboresha kiwango chake ndani ya uwanja.
Arsenal, ambayo ipo sokoni kusaka huduma ya straika wa viwango vya dunia kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi na kwa muda mrefu imekuwa ikivutiwa na Isak. Liverpool nayo imeibuka kufukuzia saini ya straika huyo, ikihitaji staa wa maana ili aje kumbadili Darwin Nunez, ambaye kwa sasa amewekwa sokoni na wababe hao wa Anfield.
Hata hivyo, Newcastle United haipo kwenye presha ya kumpiga bei straika huyo na kwamba yenyewe itafungua milango ya kutokea kama tu itawekewa mezani mkwanja unaoanzia Pauni 150 milioni.
Isak, ambaye mkataba wake wa sasa bado umebakiza miaka mitatu hana hasira zozote za kulazimisha kuhama. Geremi alisema kitu pekee ambacho kinaweza kuzisaidia Arsenal na Liverpool kwenye mawindo yao ya straika huyo ni kama mwenyewe ataamua kulazimisha uhamisho ili akacheze kwenye timu nyingine msimu ujao.
“Kitu cha kwanza, Newcastle inahitaji kubakiza wachezaji wake bora kwa gharama zote,” alisema Geremi.
“Sina hakika kama Newcastle itamuuza tu Isak kwa dau lolote, lakini itakuwa ishu kama mchezaji mwenyewe ataamua kulazimisha uhamisho.”
Baada ya kushinda taji la Kombe la Ligi mwaka huu na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, kiungo wa zamani wa Chelsea na Camerooni, Geremi anaamini Newcastle sasa ipo kwenye viwango sawa kama Liverpool na Arsenal.
Kwenye ishu ya kusaka mastraika, Arsenal imeweka ubaoni pia majina ya Benjamin Seskso na Viktor Gyokeres, huku Liverpool yenyewe ikiwa imesajili kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz kwa ada ya Pauni 116 milioni.