Abidal aibuka kudai hajafa
Muktasari:
- Abidal, 46, aliripotiwa kuwa na saratani ya ini wakati anacheza Barcelona 2011, lakini alifanyiwa upasuaji na kuondoa tatizo hilo mwaka huohuo.
BARCELONA, HISPANIA: BEKI wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa, Eric Abidal amelazimika kutoka hadharani kukanusha taarifa zinazozagaa mitandaoni kwamba amefariki dunia.
Abidal, 46, aliripotiwa kuwa na saratani ya ini wakati anacheza Barcelona 2011, lakini alifanyiwa upasuaji na kuondoa tatizo hilo mwaka huohuo.
Baadaye alifanyiwa upasuaji wa kuwekewa ini jingine 2012 kabla ya kurudi kuichezea Barcelona mwaka mmoja baadaye. Abidal alizichezea pia Monaco, Lille, Lyon na Olympiacos na aliitumikia timu ya taifa ya Ufaransa mara 67.
Uvumi uliokuwa unazagaa wikiendi iliyopita kwenye mitandao ya kijamii ulidai kwamba Abidal amefariki dunia baada ya kutokea tatizo kwenye ini lake alilobadilishwa 2012.
Lakini, Abidal alitumia ukurasa wake mwenyewe huko mtandaoni na kuweka mambo sawa.
“Kuna taarifa hazipaswi kabisa kuwepo,” alisema mchezaji huyo alipoandika kwenye ukurasa wake wa Instagram. “Nipo hapa na familia yangu na kila kitu kipo vizuri. Heshima ni muhimu. Familia yangu ipo hapa na watoto wangu wapo na mimi.
“Kwa kusema kweli, nipo vizuri, nipo hai na afya. Nashukuru kwa meseji zenu za sapoti na kuguswa. Hebu tuangalie mambo mengine muhimu.”
Abidal pia alikuwa mkurugenzi wa michezo wa Barcelona kati ya 2018 na 2020 baada ya kutundika daruga zake. Kwa ujumla wake, Abidal ameshinda mataji 15 katika kipindi chake alichokuwa Nou Camp. Kwenye maisha yake ya soka alicheza pia Ugiriki kwenye kikosi cha Olympiacos na sasa ni mkurugenzi wa michezo wa klabu ya Al Wasl Sports Club ya Falme za Kiarabu.