
Muktasari:
Mourinho alishuhudia kikosi chake kikitoa sare ya mabao 2-2 na PSG na kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya pambano la kwanza kumalizika kwa sare ya 1-1 jijini Paris. Anaamini kuwa wachezaji wake walishindwa kukabiliana na presha ya PSG.
UKIONA Jose Mourinho amekuwa mpole basi ujue amenyanyua mikono juu kwa alichokiona. Kile ulichokiona wewe basi na yeye amekiona hicho hicho, amekiri PSG walistahili kushinda na kupita.
Mourinho alishuhudia kikosi chake kikitoa sare ya mabao 2-2 na PSG na kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya pambano la kwanza kumalizika kwa sare ya 1-1 jijini Paris. Anaamini kuwa wachezaji wake walishindwa kukabiliana na presha ya PSG.
Staa wa PSG, Zlatan Ibrahimovic, alitolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi, Bjorn Kuipers, baada ya kuonekana kumchezea rafu mbaya kiungo wa Chelsea, Oscar ingawa katika picha za marudio rafu hiyo haikuonekana kuwa mbaya.
Hata hivyo, licha ya kucheza pungufu kwa muda mrefu, PSG ilikuwa timu bora uwanjani na kufanikiwa kufunga mabao mawili ya kichwa kupitia kwa mabeki wake wa kati, Wabrazili David Luiz na Thiago Silva.
“PSG ilistahili kushinda. Unaposhindwa kulinda kona mbili na kufungwa mabao mawili haustahili kushinda. Wakati timu inaposhindwa kuhimili presha ya timu ambayo haina mchezaji mmoja tena ukiwa nyumbani, na uwanja haukubali kwamba timu inabidi imiliki mechi na inataka kwende mbele kushinda...Hatukuweza kumudu presha,” alisema Mourinho.
“Kwao ilikuwa rahisi. Watu 10, muundo wa ulinzi, mistari miwili ya watu wanne, unasubiri kona au mipira ya adhabu. Kiakili kwa wao hawakuwa na cha kupoteza. Walikuwa na uzoefu, walikuwa wazuri. Walistahili.” Mabao ya Chelsea yalifungwa na Gary Cahill na Eden Hazard.
“Ni wazi kabisa kuwa wachezaji wangu hawakuweza kwenda sambamba na presha yao. Kwa kiwango cha mchezaji mmoja mmoja hatukuwa wazuri. Unaporuhusu mabao mawili ya kona, ni wazi kwamba umekosa umakini, umekosa uwajibikaji katika kukaba na nafasi ya kuimiliki. Kwa hiyo tulistahili sare hii, samahani kwa kipigo hiki.”
Mourinho alikiri kwamba alizungumza na wachezaji wake mara baada ya kipigo hicho na akaongeza kuwa angetumia saa 24 zilizofuata kufanya uchambuzi wa namna walivyopoteana katika pambano hilo.
“Nataka kujadili tulivyopoteza kwa njia za utulivu. Nataka kujua jinsi walivyojisikia mwishoni. Kiwango chetu hakikuwa kizuri. Niliwaambia hakukuwa kipindi cha kuzungumzia mechi hii. Lakini kwangu ilinishangaza. Nimeudhika. Lakini ukweli wa kwanza ni kwamba tulistahili kupoteza. Uchambuzi utafuta,” aliongeza.