Willian afichua jambo Arsenal

LONDON, ENGLAND. MAMBO yamekuwa magumu kwa nyota wa Brazil, Willian tangu alipojiunga na Arsenal na sasa mwenyewe amekiri kuwa anapita katika nyakati ngumu huku akifichua chanzo cha kufanya kwake vibaya.

Willian ambaye amejiunga na Arsenal akiwa mchezaji huru mara baada ya kumaliza mkataba wake na Chelsea baada ya msimu uliopita, amedai kuwa kuchelewa kumudu maisha ndani ya Arsenal ndio kumemfanya ashindwe kutamba akiwa na jezi za klabu hiyo. Katika mechi 18 alizoichezea Arsenal tangu alipojiunga nayo, hajafunga bao lolo huku akipiga pasi tatu tu zilizozaa mabao tena katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England waliocheza dhidi ya vibonde, Fulham.

Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 32 amefichua kuwa hadi sasa anahangaika kumudu mazingira ya Arsenal jambo ambalo limemfanya ashindwe kutoa mchango mkubwa kwa timu hiyo ambayo ana mkataba nayo wa miaka mitatu.

“Ni kweli haijawahi kuwa rahisi kubadili klabu hasa baada ya kuichezea kwa muda mrefu. Nilikuwa Chelsea kwa miaka saba kabla sijaja Arsenal na baada ya hapo unakutana na klabu mpya, watu wapya na falsafa mpya. Mambo ni tofauti hivyo naendelea kuzoea ila najisikia vizuri. Naendelea kujifunza mengi ikiwemo falsafa mpya ya soka. Kila mmoja ni mkubwa hapa. Nafahamu naweza kuimarika zaidi na bila shaka kiwango changu ndani ya uwanja kinaweza kuwa bora zaidi,” alisema Willian.

Willian aliongeza kuwa licha ya kutokuwa na kiwango cha kuridhisha ndani ya timu hiyo, kocha Mikel Arteta bado ameendelea kuwa na imani naye jambo ambalo linamuongezea hali ya kujiamini.

“Kiukweli tunazungumza mambo mengi pamoja na nafahamu kwamba ninapata sapoti yake kubwa.Siku zote ninajitahidi kufanya vizuri na niko sawa hivi sasa.

Hilo ni jambo kubwa kwangu na kuwa na sapoti kubwa ya klabu najua natakiwa kufanya kazi kwa bidii, kujitolea kila nilichonacho mazoezini kujaribu kujiimarisha. Hiyo ndio njia pekee ya kurudi katika kiwango bora,” alisema Willian. Willian katika siku za hivi karibuni amejikuta akipoteza nafasi katika kikosi cha kwanza cha Arsenal.