Koulibaly amponda bosi wa Napoli

Koulibaly amponda bosi wa Napoli

LONDON ENGLAND. BEKI wa Chelsea, Kalidou Koulibaly amemzodoa bosi wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, baada ya kusema wazi kuwa hatasajili tena wachezaji kutoka Afrika.

Bosi huyo alisema atasajili wachezaji kutoka Afrika iwapo watakubali kutowakilisha timu zao za taifa, katika Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).

Kwa mujibu wa bosi huyo anaamini timu zinapata hasara, kwani zinalazimika kutoa mishahara ya bure licha ya kutokuwepo kwa muda wa mwezi mmoja michuano hiyo ikianza.

Lakini Koulibaly amechukizwa na kauli ya bosi wake huyo wa zamani, akisisitiza timu za taifa kutoka Afrika zinatakiwa kupewa heshima.

“Hayo ni mawazo yake lakini kwa upande wangu, ni muhimu kumpa heshima kila mtu, nimebeba AFCON wakati nipo Napoli, walikuwa na wakati mgumu kipind chote ambacho hatukuwepo kwenye timu, ninachotaka ni heshima kwa Timu za Taifa za Afrika, kama nahodha wa Senegal sijapendezwa na kauli hii” alisema Koulibaly.

Bosi wa Napoli alizua gumzo mtandaoni baada ya kauli yake hiyo, hata hivyo, akasisitiza haimaanishi kwamba anawachukia wachezaji kutoka Afrika.

“Niliwaambia wasizungumze na mimi kuhusu ishu za Afrika, lakini hamaanishi kama nawachukia, nawapenda wachezaji wa Afrika, lakini ni ujinga klabu inatoa mishahara ya mwezi mzima bure, muda ukifika wanaondoka kushiriki AFCON,” alisema bosi huyo.

Koulibaly amejiunga na Chelsea akitokea Napoli kwa kitita cha Pauni 34 milioni, kama mbadala wa Antonio Rudiger aliyetimkia Real Madrid.