ZICO: ZOO KERICHO KUSHUSHWA, IMETUOKOLEA

KOCHA Zedekiah ‘Zico’ Otieno anasema kuwa ile sakata ya match-fixing iliyowakuta Zoo Kericho, imewaokolea sana klabu yake KCB kwenye harakati zao za kusaka ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Ligi hiyo ya FKF-PL inarejea kesho, Tusker FC wakiwa wangali kileleni kwa alama 33 baada ya mechi 16 huku KCB wakiwafuata katika nafasi ya pili kwa alama 29 baada ya mechi 15.
Mechi yao  KCB ya kwanza baada ya kurejea kwa ligi hapo kesho, itachezwa Jumamosi wiki hii na itakuwa dhidi ya wapinzani wao wa karibu Tusker FC.
Na huku akiwa anakiandaa kikosi chake kuwavaa Tusker, kocha Zico anasema sasa hivi wana afueni kubwa kuelekea mechi hiyo kwa sababu masaibu ya Zoo Kericho yameishia kuwafaa wao.
FIFA iliamuru Zoo Kericho ishushwe daraja hadi divisheni ya tatu baada yua sakata la upangaji matokeo mechi.
FKF ilitii amri na kuondoa Zoo kwenye ratiba mpya ya mechi zijazo. Lakini pia klabu zote zilizokuwa zimecheza dhidi ya Zoo zilipoteza alama hizo ikiwemo Tusker.
“Mwanya uliokuwa kati yetu na Tusker umepungua na sasa tofauti kati yetu ni alama nne pekee. Hii ni baada ya sisi pamoja na wao Tusker kupoteza alama dhidi ya Zoo Kericho zilizoondolewa kufuatia uamuzi wa kuwashusha daraja.” Zico katanguliza.
Hapo ndipo furaha yake Zico iliko kwani sasa anasema itakuwa rahisi kuwafikia Tusker na hata kuwapindua kileleni.
“Hii ina maana kuwa sasa kibarua chetu kuwafikia sio ngumu kama ilivyokuwa hapo awali. Najua tukipambana kwa namna tulivyofanya tulipoanza ligi, tutawang’oa kileleni Tusker.”  Zico kaongeza.
Kabla ya Zoo Kericho kuchujwa kwenye ligi kuu, Tusker walikuwa na pointi 36. Alaka tatu zilizotokana na ushindi wao wa 2-1, Janauri 2021, ziliondolewa baada ya Zoo kuchujwa.
Kwa upande wa KCB waliondolewa alama moja pekee kutokana na sare yao ya 1-1 dhidi ya Zoo  kwenye mechi iliyochezwa Machi 2021, ikiwa ni siku tano kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza lockdown.