Zico: Tuko sawa, sisajili mtu

KOCHA Zedekiah ‘Zico’ Otieno hatafanya usajili wowote dirisha dogo la usajili lilofunguliwa mwezi huu kwa kuhofia kuvuruga momentamu nzuri iliyopo kwa sasa KCB.

Kocha huyo mzoefu ana matumaini makubwa ya kutwaa taji lake la kwanza la ligi kuu msimu huu akiwa na KCB baada ya kuikosa kosa msimu uliopita.

KCB walikuwa mbioni kushinda ubingwa wa msimu wa 2020/21 ila wakaishia kuboronga kuelekea mwisho wa msimu na kuwaruhusu Tusker kuibuka mabingwa wakiwapiku kwa pointi tatu tu.

Raundi hii wameanza vizuri tena na kikosi kile kile cha msimu uliopita ingawaje Zico alifanya usajili mdogo kabla ya msimu huu kuanza.

“Kwa sasa nina kikosi kizuri chenye uwezo wa kutoa ushindani, idara zote zimejitosheleza kwa hiyo sioni sababu za kufanya usajili katikati mwa msimu. Nisingependa kuvuruga kasi tuliyonayo sasa sababu mimi sio mtu ninayeamini kujeli. Napenda nikimleta mchezaji moja kwa moja aanze kuonyesha kiwango. Wakati mwingine hii inakuwa ngumu hasa unaposajili kwa kurupuka badala ya kumpata mchezaji sahihi,” Zico anasema.

Zico pia anasema KCB ina utaratibu wa kuheshimu mikataba ya wachezaji wake hadi inapofika tamati.

“Wachezaji wote nilio nao mikataba yao bado ipo hai na hatuwezi kuzivunja ili kuwatengenezea nafasi wapya. Ila kama mchezaji atapata dili aondoke basi nitahitaji kujaza pengo hilo,” ameongeza.

Jumapili ya wiki hii KCB wanaokamata nafasi ya pili kwenye ligi watachuana na vinara Kakamega Homeboyz.