Zico, Aussems wazusha noma

KOCHA wa AFC Leopards, Patrick Aussems, ameileta juu Kamati ya Mpito Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kufuatia uamuzi wao wa kuahirisha tena msimu mpya 2022/23 wa Ligi Kuu Kenya.
Kwa mara ya pili, Kamati hiyo iliyokuwa imeratibu FKFPL kuanza Agosti 27, iliahirisha hadi Septemba 10 na tena kusongeza mbele kwa wiki mbili zaidi.
Hatua hiyo imemkoroga nyongo kocha Aussems na kama ilivyo kawaida yake, amefungua roho na kuwapasha.
“Hii ni kunikosea heshima kama kocha. Tumekuwa tukijiandaa kwa kutegemea tarehe walizotupa za mwanzo wa msimu lakini sasa wanasema tusubiri tena kwa wiki mbili zaidi. Hii ni dharau. Pengine makocha wengine wamechukulia poa uamuzi huo lakini mimi ni kocha pro, nina utaratibu wa kufanya kazi ninaouheshimu na ninapendelea chombo kama hiki kuonyeshe u-pro kwenye utekelezaji wa majukumu yake,” Aussems kaja juu.
Kulingana na Aussems, panga pangua hiyo ya Kamati haina tija kabisa na inachangia kuvuruga utendaji wake akilazimika kubadilisha tena utaratibu wa mipango aliyokuwa nayo.
Mtazamo wake umeungwa mkono na kocha wa KCB, Zedekiah ‘Zico’ Otieno ambaye naye pia kacharuka akitaka utaalamu uzingatiwe na kamati iwache kuvuruga ratiba zao za maandalizi.
“Waache kutuzengua, wanatuvurugia mipango na ratiba. Tulianza maandalizi yetu tukiwa na Agosti 27 kichwani, wakabadilisha na kusema ligi itaanza Septemba 10 sasa wamesogeza tena hadi Septemba 24, mbona haeleweki, alihoji Zico.
Wakati Aussems na Zico wakikwazika, kocha wa Gor Mahia, Johnathan McKinstry kabambika na mabadiliko hayo.
Muingereza huyo kadai timu yake haijaiva poa hivyo wiki hizo mbili zitampa muda wa kutosha kuwaweka sawa.
“Tulichelewa kidogo kuanza maandalizi yetu ukizingatia kuwa ndio tupo kwenye wiki ya tatu tangu tumeanza pre-season yetu. Maandalizi mazuri ya mwanzo wa msimu huhitaji angalau wiki sita hivyo mabadiliko hayo, imetujenga sana,” alisema McKinstry.