Wakenya wabeba  ndoo Coco Beach

Muktasari:

  • Mashindano hayo yaliyofanyika viwanja vya Coco Beach, jijini Dar es Salaam yalihusisha klabu sita za wanaume kutoka Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania zilitawaliwa na klabu hizo mbili za Kanda ya Pwani zilizofika fainali. 

TIMU za Kenya, Kwale Kings na Kilifian HC juzi zilidhihirisha kuwa bora katika mchezo wa mpira wa mkono wa ufukweni baada ya kutawala mashindano ya TAHA Open Handball Championship yaliyohusisha klabu za Kanda ya Tano barani Afrika.
 
Mashindano hayo yaliyofanyika viwanja vya Coco Beach, jijini Dar es Salaam yalihusisha klabu sita za wanaume kutoka Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania zilitawaliwa na klabu hizo mbili za Kanda ya Pwani zilizofika fainali. 

Kwale Kings iliongoza Kundi A ilihali Kilifian ikatamba kileleni Kundi B na kwenye nusu fainali, Kwale iliifunga Ngome ya Tanzania kwa seti 2-0 (15-12, 17-11), huku Kilifian ikaiangusha JKT ya Tanzania pia kwa seti 2-0 (11-9, 16-8).
 
Katika mechi ya fainali iliyohusisha miamba hiyo ya Kenya na iliyovutia mashabiki wengi, Kwale Kings iliishinda Kilifian kwa mipigo ya penalti ya 3-2.
 
Katika muda wa kawaida, timu hizo zilifungana seti 1-1. Kwale iliongoza 16-15 kwenye kipindi cha kwanza, lakini Kilifian ikasawazisha kipindi cha pili kwa 6-2. Ikabidi penalti zichukuliwe na Kwale wakapata ushindi. 

Kocha wa Kwale Kings, Abdalla Chaka amesema alitarajia ushindi wa vipindi vyote viwili, lakini wapinzani wao wamekuwa bora zaidi kipindi cha pili na kulazimisha mchezo kuamuliwa kwa penalti. 

"Hata hivyo, sikuwa na wasiwasi wowote wakati wa mipigo ya penalti nilijua juhudi za wachezaji wangu zitatupa ushindi tuliostahili," aloisema Chaka, huku Kocha wa Kilifian, John Karisa alikiri awali walitegemea kushinda taji hilo lakini ni bahati haikuwa yao hasa wakati wa mipigo ya penalti. 

"Wachezaji wangu wamekuwa wenye kujituma na nilikuwa na imani kubwa kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya ndugu zetu wa Kwale Kings lakini bahati iliwaendea wapinzani wetu," alisema Karisa. 

Mwanakamati wa Shirikisho la Handiboli la Kenya anayesimamia handiboli ya ufukweni, Caroline Nyadiero ametoa pongezi kwa timu hizo za Kenya, Kwale Kings na Kilifian kwa kuhakikisha zote zimefika fainali na kuibuka washindi wa nafasi mbili za kwanza. 

"Ni jambo la kuvutia kuona timu zetu mbili ndizo zilikutana katika fainali na kuihakikishia mojawapo ya timu ya Kenya kuwa washindi wa mashindano hayo tuliyoalikwa na Shirikisho la Handiboli la Tanzania (TAHA)," alisema Nyadiero.