Ushindi wampa jeuri Mkenya Singida Black Stars
Muktasari:
- Singida ilipata ushindi huo jana kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma kupitia mabao ya Mossi Ndimumwe, Horso Muaku na nahodha Kennedy Juma, huku Raizin Hafiz akiwafungia wenyeji bao la kufutia machozi na kuifanya ifikishe pointi 15 ikishika nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu.
USHINDI wa mabao 3-1 iliyoupata Singida Black Stars ikiwa ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar, umempa jeuri kocha Mkenya, David Ouma akiamini kwamba umeiongezea timu morali kwa ajili ya mechi ijayo itakapoifuata Namungo, mkoani Lindi.
Singida ilipata ushindi huo jana kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma kupitia mabao ya Mossi Ndimumwe, Horso Muaku na nahodha Kennedy Juma, huku Raizin Hafiz akiwafungia wenyeji bao la kufutia machozi na kuifanya ifikishe pointi 15 ikishika nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu.
Alhamisi Singida itaifuata Namungo iliyotoka kupasuka kwa bao 1-0 mbele ya Yanga ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Majaliwa, Ruangwa ikiwa ni mfululizo wa mechi za viporo vya Ligi Kuu, huku Ouma ambaye ni raia wa Kenya akitamba kwamba anaamini wataendeleza wimbi la ushindi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma ameisifu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwa kufanyia kazi dosari zilizokuwapo za kushindwa kutumia kila nafasi wanayotengeneza, lakini akiitaka muendelezo huo uendelee kwa kila mechi iliyopo mbele yao kufanikisha malengo ya msimu huu wa 2025-2026.
"Kuna mabadiliko makubwa katika safu ya ushambuliaji, mechi mbili mfululizo sasa tunashinda mabao kuanzia matatu. Tulianza na mechi ya Kombe la CRDB tukiibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Copco FC na leo (juzi) tukiwa ugenini mechi ya ligi tumepata ushindi kama huo," amesema Ouma na kuongeza;
"Ni mwendelezo mzuri, lakini bado tunatakiwa kufanyia kazi udhaifu wa kuruhusu nyavu zetu kuguswa, tukifunga tunatakiwa kulinda ushindi na kwa kutoruhusu mpinzani kufika mara kwa mara langoni mwetu."
Akizungumzia mechi ya Alhamisi dhidi ya Namungo, Ouma amesema haitakuwa rahisi kutokana na aina ya mpinzani wanayeenda kukutana naye akiwa nyumbani na pia ametoka kuangusha pointi tatu, lakini wamejiandaa kupata matokeo mzuri.
"Hautakuwa mchezo rahisi, mbinu bora na timu iliyojiandaa vizuri ndivyo itakayoibuka na ushindi kwa upande wetu, tunazihitaji pointi tatu bila kujali tunacheza kwenye uwanja gani, matokeo popote yanapatikana, kikubwa ni maandalizi mazuri na wachezaji kutambua umuhimu wa mchezo."
Ouma amesema hakuna timu rahisi, hivyo wanaiheshimu Namungo na anatambua ubora wa benchi la ufundi la timu hiyo, hivyo ataenda akiwa na nidhamu kuanzia kikosi hadi mbinu sahihi ili aweze kuendeleza na ushindi.