Trucha, Logarusic stori hazitofautiani

NAFASI kwenye msimamo wa Ligi Kuu Kenya ambayo kocha mpya wa AFC Leopards, Tomas Trucha, ameikuta timu hiyo haina tofauti na nafasi ambayo Zdravko Logarusic aliikuta Kenya Police FC alipokabidhiwa mikoba.

Macho sasa yapo kwa Trucha kama anaweza akawapa uhai mabingwa mara 12 FKFPL, Ingwe, design ambayo Logarusic anavyozidi kuibadilisha Police FC tangu kumrithi mzawa Francis Baraza.

Logarusic, raia wa Croatia, aliikuta Police FC katika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa FKFPL ikiwa na pointi tatu tu.

Chini ya kocha Baraza, magalacticos hao wa FKFPL walikuwa wamecheza mechi nne pasipo kushinda mchezo wowote na gemu ya mwisho kwa Baraza ilikua sare ya mabao 2-2 dhidi ya Leopards.

Lakini tangu kutua kwa Logarusic, Police FC imeshinda mechi mbili back-to-back dhidi ya Bidco United na Nairobi City Stars, na kupanda hadi nafasi ya tano wakijikusanyia pointi tisa.

Mafans wanaamini mabadiliko kwenye benchi la ufundi ambayo uongozi wa Ingwe umefanya wiki iliyopita yataendana na matokeo mazuri uwanjani kama tu yanavyoshudiwa katika timu ya Police FC.

Presha ya mafans imepelekea Leopards kuachana na kocha Tom ‘Gazza’ Juma baada ya mechi sita tu za ligi na nafasi yake kuchukuliwa na Trucha.

Trucha anaikuta Ingwe ikiwa nafasi ya 17 na pointi nne kwenye msimamo wa FKFPL pasipo na ushindi wowote huku mchezo unaofuata ukiwa wikendi hii baada ya kukamilika international break ambapo Ingwe wanasafiri kuelekea jijini Mombasa kuwakabili wenyeji Bandari FC.

Kocha huyo raia wa Jamhuri ya Czech anayeshikilia leseni ya ukocha ya UEFA Pro, amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea timu ya Kelantan United ya nchini Malaysia.

Trucha anarudi tena Ingwe ambayo aliifundisha kwa mwezi moja kabla ya kujiuzulu mwaka 2020 kwa kile alichokitaja kuhofia usalama wake kufuatia meneja wake, Prince Channis, kutishiwa maisha na watu waliyodai ni mafans wa Ingwe.

Safu mpya ya benchi la ufundi Ingwe litahusisha Fred Ambani anayeendelea kubaki kama kocha msaidizi, Haggai Azande ni kocha mpya wa makipa akimrithi Lawrence Webo na nahodha wa zamani Bernard Mang’oli ndiye meneja mpya wa timu akichukua nafasi ya Albert Wesonga ambaye amepanda cheo na sasa ni Ofisa Mtendaji Mkuu.