Stars piga Wasudani tupande ranki FIFA

TOP 100 kwenye viwango bora vya soka duniani vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) inawezekana endapo timu ya taifa, Harambee Stars, itaibuka na ushindi leo Jumanne dhidi ya Sudan Kusini.

Timu hizi mbili zitashuka katika uga wa Moi Kasarani jijini Nairobi kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya kirafiki itakayochezeshwa na refa mzoefu Mnyarwanda Twagirumukiza Abdoulkalim akisaidiwa na raia wenzake Justin Karangwa na Raymond Bwiriza huku mwamuzi wa akiba ni Mkenya Josephine Wanjiku na kamishna wa mechi akiwa Francis Oliele.

Harambee Stars chini ya kocha Engin Firat watawavaa Bright Stars takribani siku tano baada ya kuwashangaza wenyeji wa Kombe la Dunia mwaka jana, Qatar, wakiwachapa kwao mabao 2-1.

Matokeo hayo yanatarajia kuboresha viwango vya ubora wa soka vya FIFA vitakavyotoka Septemba 21 mwaka huu ikizingatiwa kwasasa hivi Stars wapo nafasi ya 105 na waliwafunga Qatar ambao kwenye orodha ya FIFA wapo nafasi ya 59.

Lakini nafasi hiyo itaboreka zaidi iwapo vijana wa kocha Firat watawatandika Sudan Kusini ambao kwenye viwango vya ubora wa soka duniani wapo nafasi ya 167.

Nafasi ya juu zaidi waliyowahi kukamata Harambee Stars ilikua 68 hii ikiwa ni Desemba mwaka 2008 wakati Julai mwaka 2007 ulikuwa mwezi mbaya wakishika nafasi ya 137.

Morali ya Stars ipo juu kuelekea gemu yao dhidi ya Sudan Kusini waliyochezea kichapo cha mabao 4-0 mikononi mwa Mali wiki iliyopita mchezo wa Kundi G kufuzu Kombe la Afrika mapema mwakani nchini Ivory Coast.

Straika wa Sudan Kusini aliyejiunga na magalacticos wa FKFPL Kenya Police FC, Tito Okello, alisema wanajihisi kama wako nyumbani baada ya timu hiyo kuwasili juzi Jumapili kwa mechi hiyo ya kirafiki.

“Hii ni kama mazoezi mengine, tulipata somo kutoka gemu dhidi ya Mali na tupo hapa kurekebisha baadhi ya makosa,” alisema Okello na kusisitiza kuwavaa Harambee Stars itakuwa gemu kubwa kwao.

Mara ya mwisho timu hizi mbili kukutana ilikua Machi 13, 2021 ndani ya dimba la Nyayo jijini Nairobi na Harambee Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Elvis Rupia aliyejiunga na Singida Fountain Gate ya Bongo akitokea Police FC.

Harambee Stars wanatumia mechi hii na ile ya wiki iliyopita dhidi ya Qatar kujiandaa na ngarambe za kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2026 wakiwa wamepangwa kundi moja na Ivory Coast, Gabon, The Gambia, Ushelisheli na Burundi.

Baada ya ushindi dhidi ya mabingwa wa Asia, nahodha Michael Olunga aliiomba Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuhakilisha timu inaendelea kucheza mechi za kirafiki dhidi ya timu kubwa.