Sportpesa yapiga jeki Raga

Meneja wa Chama cha Raga cha Kenya, Sasha Mutai (Kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa, Ronald Karauri (Kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Kenya Sevens na maafisa wengine wa KRU wakati wa hafla ya kuwasilisha hundi mnamo Juni 29, 2023.

Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa, Mheshimiwa Ronald Karauri ameahidi kuwekeza kwa kutoa misaada kwa timu za raga nchini pamoja na timu ya taifa ya mchezo huo.
SportPesa imethibitisha kujitolea kwake kusaidia Shujaa kurejesha fahari na utukufu wao ‘uliopotea’ baada ya kushushwa daraja kutoka kwa mfululizo wa HSBC katika mashindano ya dunia ya raga yaliyofanyika mapema mwezi huu nchini Ufaransa na Uingereza.

"Tutaendelea kuwekeza katika timu yetu ya taifa na kutoa msaada zaidi kwa vilabu vya ndani. Tuna imani tukiwa na uongozi sahihi tutaona vipaji chipukizi vikitoka kwenye mzunguko wa SportPesa wa wachezaji saba kila upande. Msaada wetu na kujitolea kwetu kunapaswa kuwa nguvu ya kuongoza kufanya maono haya kuwa kweli," alisema Karauri.
Ili kusaidia kukuza vipaji ndani ya nchi kama malisho kwa timu ya taifa, SportPesa imechukua udhamini wa mwaka huu wa taji la mzunguko wa raga ya wachezaji saba kila upande, unaoitwa 'SportPesa National 7s Circuit'.

Kulikuwepo na sintofahamu katika wiki kadhaa zilizopita, iwapo SportPesa itaondoa ushirikiano wake na shirikisho la raga nchini.
Alikuwa akizungumza wakati wa kifungua kinywa na Shirikisho la Raga la Kenya, wachezaji wa Shujaa na timu ya taifa ya Kenya ya wanawake ya Lioness, pamoja na wawakilishi wa timu zinazoshiriki katika mzunguko huo.
Katika mpango huo mpya, SportPesa inaingiza Sh15,000,000 kusaidia mzunguko wa raga wa ndani kila mwaka, kwa miaka mitatu.

Hii itaona uungwaji mkono kwa muungano na vilabu sita vinavyoandaa mzunguko huo, kuanzia na Dala 7 za wikendi hii mjini Kisumu na kufuatiwa na Mombasa na zingine nne.
"Kama ofisi mpya, tunajua hatimaye tutarejea kwenye jukwaa la dunia haraka iwezekanavyo. Tunawapongeza SportPesa kwa sababu safari yao ya mchezo wa raga inasonga mbele, huu ni mwanzo wa mambo makubwa yajayo, tukianza na mashindano ya ndani ya Sportpesa,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Raga cha Kenya, Alexander Mutai.

SportPesa itatoa kwa kila klabu itakayoshiriki Sh1,000,000 ili kusaidia kuweka pamoja mashindano yenye mafanikio. Washiriki wa Mzunguko wa SportPesa 7s pia watakuwa na zawadi nzuri ya pesa za hadi Sh2,500,000 kupigania mzunguko mzima.
SportPesa pia itaingiza Sh22,000,000 kwenye timu ya ili kusaidia kujijenga na kujiandaa kurejea katika mashindano ya kimataifa.