Soka Kenya lampa homa Origi

ALIYEKUWA kipa wa Harambee Stars, Arnold Origi, amesema Kenya kufuzu Kombe la Dunia 2030 zitasalia ndoto za alinacha ikiwa mabadiliko makubwa hayatafanyika haraka upesi.
Kauli ya Origi inatokana na tamko la Baraza la Mawaziri chini ya Rais William Ruto kukusudia kuwasilisha maombi kuandaa Kombe la Afrika 2027 kwa kushirikiana na mataifa ya Afrika Mashariki wakiwa na malengo ya kufuzu Kombe la Dunia 2030.
Origi mwenye umri wa miaka 39 alisema taifa bado lina safari kubwa kabla ya kufika levo za kuwa washindani wa kisawasawa.
“Ufanisi wa soka hauna njia ya mkato. Ili kukuza vipaji tunahitaji miundo mbinu ila hatuna. Vipaji pekee havitoshi. Hivi ndivyo mataifa yaliyoendelea yanavyofanya. Kama kweli tuna nia ya kuwa bora, basi tuanza kwa kubotresha viwango vya miundo mbinu zetu,” alishauri.
Suala lingine linalomkwazwa Origi ni idadi ya akademi za soka zinazoibuka ambazo anasisitiza asilimia kubwa, zimechipuka kwa malengo ya kibiashara zaidi na wala sio kuvilea na kunoa vipaji.
“Akademi nyingi za soka hapa nchini hazina makocha wenye mafunzo sahihi na hiyo ni hatari sababu wachezaji chipukuzi wanaishia kukosa zile miundo misingi mahususi ya mwanasoka. Nazishauri akademi hizi kuajiri makocha wenye vigezo,” alisema kipa huyo wa zamani wa Harambee Stars ambaye amehitimu levo ya ukocha kiwango cha UEFA B.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu alipoachana na soka, Origi amekuwa akipokea mafunzo ya ukocha huku pia akisimamia AFRI Child Sports Academy iliyopo Oshwal Community Centre, Nairobi.