SIMBA WARUKA BEI YA ONYANGO PIRATES

Tuesday April 27 2021
ONYANGO FULL PICHA
By Thomas Matiko

KLABU ya Simba SC, imeruka zile tetesi za kuwa imemwekea beki wa Harambee Stars dau lisilopungua Sh100 milioni kwa klabu yeyote inayoanuwia kumsajili.
Tetesi hizo zilivumishwa na msemaji wa Simba, Haji Manara ambaye wiki iliyopita alifichua miamba wa soka kutoka Afrika Kusini, Orlando Pirates walimpigia simu kuulizia uwezekano wa kumsajili beki huyo kisiki.
Katika majibu yake, Manara alidai kuwafahamisha Pirates ili kumpata Onyango mwenye miaka 28, watahitaji kuweka mezani kiasi kisichopungua dola milioni moja (Sh108, 000,000).
Hata hivyo mmoja wa Wakurugenzi wa bodi ya Simba SC, Mulamu Nghambi kafanya mahojiano na jarida moja la kule Afrika Kusini lililotaka kupata uhakika wa taarifa hizo.
Kwenye mahojiano hayo, Nghambi aliruka kauli za Manara kwa kusema sio kweli na kwamba klabu wala haijatoa mawasiliano yeyote kuhusiana na ishu ya Onyango.
“Kusema kweli sina taarifa zozote au mawasiliano ya aina yeyote kutoka Orlando Pirates kuhusu hiyo ishu. Kwa sababu hiyo siwezi kukomenti wala kusema chochote kwa sababu hatujapokea mawasiliano rasmi kutoka Orlando Pirates. Na labda niseme hivi, ni uvumi tu,” Nghambi kanukuliwa na jarida hilo la kimichezo nchini la huko S.A
Kulingana naye, Simba wamekuwa wakicheza vizuri sana msimu huu hasa katika shindano la CAF Champions League ambapo kiwango cha Joash kimekuwa kikionekana.
Kutokana na kiwango kizuri cha Joash na kikosi cha Simba kwa jumla, ni kawaida kuzuka kwa minong’ono ya aina hiyo timu inapokuwa inacheza vizuri.
“Najua ni kwa sababu timu yetu imekuwa ikicheza vizuri sana kwenye Champions League ndio maana kumekuwepo na uvumi kibao kuhusiana na wachezaji wetu. Ila mpaka sasa hamna mawasiliano yeyote yaliyo rasmia kutoka kwa klabu husika,” Ngambi kaongeza.
Wiki iliyopita Joash alithibitisha naye hajapokea taarifa zozote kutoka kwa Orlando Pirates iwe ni kupitia wakala wake au klabu.

Advertisement