Si bure Wanyama kuwalenga CF Montreal

KLABU ya CF Montreal FC imefichua chanzo cha kushindwa kumwongezea mkataba nahodha wa zamani wa Harambee Stars, Victor Wanyama, ambaye wiki mbili zilizopita alidhibitisha ataikacha klabu hiyo mkataba wake utakapofika kikomo Desemba mwaka huu.
Sasa uongozi wa klabu hiyo umefichua kwamba mazungumzo baina yao na Wanyama kuhusu kumrefushia mkataba ulifeli, baada ya mchezaji huyo kuzikataa ofa zote walizomwekea mezani.
CF Montreal inasema, ilijitahidi sana kumshawishi nahodha huyo msaidizi wa timu yao asalie nao, lakini jamaa akadinda, hii ni licha ya kwamba hadi kufikia mwaka jana, alikuwa miongoni mwa wachezaji 10 bora wenye mishahara mikubwa Ligi Kuu ya Marekani maarufu Major Soccer League (MSL).
“Sisi tulishajua zamani kwa miezi kadhaa sasa kwamba hatakuwa nasi baada ya msimu huu. Kama akiondoka, huo utakuwa ni uamuzi wake na wala sio wetu. Tumemwekea mezani ofa kadhaa na amezikataa zote,” Mkurugenzi wa Montreal, Olivier Renard kaiambia TVA Sports.
Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa mwaka jana na MLS Players Association, Wanyama anakamata nafasi ya 14 miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa.
Miongoni mwa viungo wa MLS wanaolipwa mishahara mikubwa, Wanyama anaongoza.
Kipato chake kwa mwaka ni dola za Marekani milioni 3.09 (KSh371 milioni) pamoja na bonasi na marupurupu huku mshahara tu kwa mwaka ni dola milioni 2.4 (Sh288 milioni) kwa mwaka.