Pinki pinki ponki kileleni patamu

WAZITO FC wameifanyia Tusker FC ile kitu na sasa kuna mfalme mpya kileleni mwa msimamo Ligi Kuu Kenya huku zikiwa zimebakia raundi mbili tu msimu wa 2022/23 kutamatika.

Gor Mahia walifaidika na matokeo hayo katika Uwanja wa Muhoroni, Kaunti ya Kisumu wikendi iliyopita ukizingatia walicheza kama wao walipowakabili Ulinzi Stars ndani ya uga wa Nyayo jijini Nairobi.

Tusker FC ambao ni mabingwa watetezi, walisafiri kwenda Muhoroni wakijuafika mechi yao na Wazito FC haitakuwa mteremko.

Hii ni kutokana na Wazito FC katika mechi za hivi karibuni kuwa wagumu kufungika wanapocheza nyumbani ambapo kabla ya kuwavaa Tusker FC walikuwa wamepoteza mchezo moja kati ya tano walizocheza kwenye ‘home ground’.

Ugumu wa mechi hii pia ulitokana na Wazito FC kuwa katika mstari wa kushuka daraja na salama yao ni kuhakikisha wanamaliza nafasi ya 16 ili wacheze playoff kuendelea kuweka hai matumaini ya kucheza FKFPL msimu ujao.

Wazito FC walikuwa washawatahadharisha mabingwa watetezi FKFPL kwamba watakiona cha moto na mabao mawili ya Collins Neto yaliipunguza kasi vijana wa Robert ‘Simba’ Matano ambao bao lao la kufutia machozi lilifungwa na Charles Momanyi.

Wakati Tusker FC wanalowa, wikendi ilikua bomba kwa Gor Mahia kwani mabao ya Austin Odhiambo na John Macharia dhidi ya Ulinzi Stars sio tu yaliwafanya kurudi kileleni lakini pia yalihitimisha ukame wa kucheza mechi tatu mfululizo pasipo kupata ushindi.

Kocha wa K’Ogalo, Jonathan McKinstry, aliwamiminia sifa wachezaji wake kwa kuonyesha mchezo mzuri.

“Mmeshawahi kunisikia kipindi cha nyuma nikisema kwamba hii ni timu changa na matokeo hayawezi kuja vile tunavyotaka kwasababu tunajaribu kujenga kikosi,” alisema mkufunzi huyo raia wa Ireland Kaskazini.

Kipigo cha Tusker FC kimefufua matumaini japo finyu kwa Nzoia Sugar iliyo nafasi ya tatu kwa pointi 63 kufuatia ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Nairobi City Stars hata hivyo endapo Gor itashida mechi inayofuata dhidi ya Kakamega Homeboyz basi ndoto zao kutwaa ubingwa msimu huu zitafutika.