Marathon chini ya saa mbili inawezekana

KAMA isingekuwa Eliud Kipchoge basi ni Kelvin Kiptum, wanariadha wawili waliotabiriwa mmoja wao kuvunja rekodi ya dunia mbio za marathon.

Hatimaye ni Kiptum amefanya kweli juzi Jumapili akiweka rekodi mpya ya mbio hizo za kilomita 42 katika Chicago Marathon, Marekani akivunja ile iliyowekwa na Kipchoge mwaka jana mbio za Berlin Marathon, Ujerumani.

Imemchukua Kiptum miezi 10 na hususan marathon tatu tu kuweka rekodi mpya ya dunia ya muda wa saa mbili na sekunde 35 akivunja kwa sekunde 34 rekodi ya Kipchoge.

Kiptum alijua ni nini anachokitaka Chicago Marathon alipoamua kuyapa kisogo Mashindano ya Riadha ya Dunia yaliyofanyika jijini Budapest, Hungary, pia kuwanyima uhondo mafans kumuona kwenye shindano moja na Kipchoge katika mbio za Berlin Marathon.

Kipchoge alikua amedhamiria kuvunja rekodi yake ya dunia kwenye mbio za Berlin Marathon zilizofanyika mwishoni mwa mwezi uliyopita, japo alifanikiwa kutetea taji lake akimaliza kwa muda wa saa 2:02:42 alikosa kwa dakika 1:33 kuvunja rekodi yake.

Hata hivyo, gwiji huyo alinukuliwa akisema ni suala la muda rekodi ya dunia mbio za marathon itavunjwa na kuongeza ipo siku marathon itakuwa inakimbiwa kwa chini ya saa mbili.

Imechukua wiki mbili tu, kwa Kiptum mwenye umri wa miaka 23 kutimiza alichosema Kipchoge kuhusu rekodi ya dunia mbio za marathon kuvunjwa na sasa macho ni kushuhudia mwanariadha yupi ataipunguza zaidi kwa kukimbia chini ya saa mbili.

Akiongea baada ya kuweka rekodi mpya ya dunia, Kiptum alisema alijiandaa kwa mbio hizo na lengo lake ilikua ni kuifuata rekodi ya Chicago Marathon na wala hakuwaza rekodi ya Kipchoge.

“Ninajiskia furaha sana, nilikua nimekuja kufuata rekodi ya Chicago lakini kwa bahati nzuri imekua rekodi ya dunia ambayo haikua kwenye mpango,” alisema Kiptum japo alijua kuna siku atakua mshikilizi wa rekodi ya dunia.

Mambo makubwa yanasubiriwa kwa Kiptum ikizingatiwa Chicago Marathon ndiyo lilikua shindano lake la tatu kubwa na zote ameibuka bingwa.

Alianza na Valencia Marathon nchini Hispania Desemba mwaka jana akikimbia kwa kasi na kumaliza kwa muda wa saa 2:01:53 na Aprili mwaka huu kwenye London Marathon nchini England alikosa kwa sekunde 16 kuvunja rekodi ya Kipchoge akimaliza kwa muda wa saa 2:01:25.

Kiptum alimuacha kwa mbali aliyekuwa bingwa mtetezi, Benson Kipruto, aliyemaliza wa pili kwa muda wa saa 2:04:02 akifuatiwa sekunde 30 baadaye na Bashir Abdi raia wa Ubelgiji.