Lilian asepe zake Ulaya, Vihiga Queens kusaka kipa mpya

DILI nono alilopata kipa wa Vihiga Queens na timu ya taifa ‘Harambee Starlets’, Lilian Awour Onyango, linafungua milango kwa nyota kibao wa timu hiyo kusaka malisho mapya kwa klabu zilizopiga hatua soka la wanawake.

Lilian anatarajiwa kuondoka nchini Jumapili kuelekea Ufaransa kujiunga na ASJ Soyaux-Charente inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Vihiga Queens ilithibitisha kuondoka kwa kipa huyo hodari kupitia taarifa ya klabu ikisisitiza kamati ya utendaji Vihiga Queens imebariki Lilian kujiunga na ASJ Soyaux-Charente maarufu Soyaux Women Football Club.

Aidha taarifa hiyo ya Vihiga Queens ilisema dili la Lilian ni moja tu miongoni mwa dili kibao za timu kubwa barani Afrika na Ulaya waliyoonesha nia ya kuwasajili.

“Ni matumaini yetu nia hizi zitageuka fursa kwa wasichana wetu ili waende wakaliteke soka la dunia,” ilisema sehemu ya taarifa ya klabu.

Straika Tereza Engesha ni mchezaji mwingine wa Vihiga Queens ambaye tetesi zinadai klabu zimeonyesha nia ya kumsajili japo hazijatajwa.

Macho ya wakala wengi yameelekezwa Vihiga Queens hususa baada ya kushiriki na kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki iliyotumika pia kufuzu michuano ya Klabu Bingwa Afrika upande wa wanawake zilizofanyika kwa mara ya kwanza nchini Misri mwaka jana.

Kipa Lilian, mbali na Vihiga Queens kupoteza mchezo wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, alitwa tuzo ya mchezaji bora, pia alikuwa katika kiwango bora timu yake ikiichapoa FAR Rabat ya Morocco mabao 2-0.

Lilian alin’gara mchezo wa mwisho wa makundi dhidi ya Rivers Angels ya Nigeria kabla ya presha kuwa kubwa na timu kupoteza mchezo huo.

Takwimu zinaonyesha katika mechi dhidi ya Rivers Angel, kipa huyo alipangua michomo 19 ikiwa ni idadi kubwa ukilinganisha na kipa yeyote kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wachezaji wengine wa Starlets wanaosakata soka la kulipwa barani Ulaya ni Essy Akida, Mwanahalima Adam na Dorcus Shikobe.

Wakati huo huo, Kocha wa Vihiga, Boniface Nyamunyamu amesema wameanza mchakato kusaka kipa mwingine kujaza pengo litakaloachwa wazi na Lilian.

‘’Sina budi kumshukuru kipa wetu huyo. Amekuwa tengemeo kubwa kwenye mechi zetu,’’ kocha huyo alisema na kumtakia mema anakolenga kuanza makao mapya.

“Kuondoka kwa wawili hao itakuwa pigo kwa timu yetu kwenye juhudi za kupigania taji la ligi kuu msimu huu lakini itakuwa nzuri kwa kupata hela,’’ alisema na kuongeza wamepania kujituma mithili ya mchwa kufukuzia taji hilo.

Vihiga imetwaa uongozi wa mapema katika jedwali la kipute hicho kwa kuzoa alama 12 baada ya kushinda mechi zote nne ambazo imeshiriki.

Gaspo Queens inashikilia nafasi ya pili kwa kuzoa alama tisa, sawa na Thika Queens na Trans Nzoia Falcons tofauti ikiwa idadi ya mabao.


Na ISIJI DOMINIC na John Kimwere