KOCHA AUSSEMS HAIAMINI INGWE YAKE

Thursday December 30 2021
ingwe pic
By Sinda Matiko

PATRICK Aussems kawaweka sawa mashabiki wa AFC Leopards kwa kuwataka wafahamu kuwa timu yao ya msimu huu, iko chini kinoma.
Huku akiendelea kupewa presha ya kubadilisha matokeo, Aussems kafungua moyo wake na kukiri kwamba kikosi alichonacho kwa sasa, hakina  uwezo wa kutoa ushindani kwenye ligi kuu ya FKF-PL.
"Sipendi kuwa mnafiki, hapa hatuna timu. Sikutegemea ningekuwa na kikosi kichanga msimu huu kama nilichonacho kwa sasa. Nilitegemea kwamba ningekuwa na baadhi ya wachezaji wangu wazoefu wa msimu uliopita. Lakini wote waliondoka na kunilazimu kuanza kusuka kikosi kingine upya na hii niliyonaiyo, haina uwezo wa kutoa ushindani," Aussems kakiri.
Mabingwa hao mara 13 wa ligi kuu, waliwapoteza wachezaji 16 wazoefu mwishoni mwa msimu uliopita.
Asilimia kubwa ya wachezaji hao waligura kutokana na hali ya msoto inayoendelea kuihangaisha klabu hiyo.
Baada yao kuondoka, Ingwe ilishindwa kutoa fedha za kuwasajili wachezaji wa viwango na kumlazimu Aussems kuwatumia wachezaji wa timu chipukizi wasio na uzoefu.
Matokeo ya kikosi hicho yamedhihirika wazi wazi, wakisajili matokeo mabaya mno. Wamepoteza mechi tano mfululizo kati ya kumi walizocheza mpaka sasa. Wametoka sare tatu na kushinda mbili tu.

Advertisement