Kisa msupa, Wanyama akataa doo

NAHODHA wa zamani wa Harambee Stars, Victor Wanyama, amefunguka sababu ya kuamua kusalia ndani ya klabu ya Montreal FC licha ya awali kukata kauli angeondoka mwishoni mwa mmwaka 2022.

Mtakaba wake ulipokuwa unaelekea ukingoni Desemba mwaka jana, Wanyama aliweka wazi hakuwa na mpango wa kuendelea kusalia Montreal FC ambayo ni klabu alijiunga nayo baada ya miaka minne akikipiga Tottenham Hotspurs.

Akizungumza na jarida la Montreal Gazette, Wanyama kafafanua sababu za kubadili gia angani na kutema ofa nono alizopokea kutoka klabu za Saudi Arabia, Uturuki na Italia.

“Mkataba wangu ulipokuwa unaelekea tamati mimi na klabu tulishindwa kufikia makubaliano mapya. Nilienda nyumbani na kuwazia jambo hilo na kisha mazungumzo na Montreal tukayaanza tena Krisimasi,” Wanyama alisema.

Kiungo huyo alisema alizipiga chini ofa kubwa ambazo zingemlipa kiasi kikubwa cha pesa kwasababu alichokitazama zaidi ni wapi familia yake itakuwa na furaha.

Wanyama kamchumbia mwigizaji staa hapa nchini Serah Teshna Ndanu ambaye tayari wamejaliwa mtoto wa kiume ambaye ana miaka miwili sasa.

Ndanu alirejea kwenye ulingo wa uigizaji mwaka jana baada ya miaka mitatu kuwa nje, na kuigiza kwenye series ya Igiza kama mhusika mkuu.