Kiptum ndiye Kipchoge mpya

ILIKUA imebaki sekunde 17 tu, Kelvin Kiptum kuvunja rekodi ya dunia mbio za marathon inayoshikiliwa na gwiji Eliud Kipchoge akitimka kwa kasi ya ajabu katika mbio za London Marathon zilizofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kiptum aliyemaliza mbio hizo akitumia muda wa saa mbili, dakika moja na sekunde 25, alijawa na furaha kiasi cha kushindwa kusema chochote kuhusiana na mbio hizo na hususan muda aliyoweka.
“Nina furaha sana kutokana na haya matokeo, sijui hata niseme nini kwasasa,” yalikuwa maneno ya Kiptum ambaye amevunja rekodi ya London Marathon ya saa 2:02:37 iliyowekwa na Kipchoge mwaka 2019.
Tayari Kiptum mwenye umri wa miaka 23 ameanza kutajwa kama mrithi wa Kipchoge aliye na umri wa miaka 38 katika mbio za masafa marefu.
Hata hivyo Kipchoge atabaki kuwa Kipchoge kutokana na mambo makubwa ambayo ameyafanya kwenye riadha hususan tangu ahamie kwenye marathon akitokea kushiriki mbio za mita 5000.
Kwa hakika Kipchoge ni G.O.A.T. wa marathon akishinda mbio zote kubwa za marathon isipokua Boston na New York na ndiye mwanariadha pekee kukimbia mbio za kilomita 42 kwa chini ya saa mbili japo hayakuwa mashindano rasmi.
Kipchoge bado hajatangaza kustaafu hivyo anaweza akashangaza wengi kadri anapoendelea kushiriki mbio za marathon huku akilenga kuwa mtu wa kwanza kushinda mbio za marathon mara tatu katika mashindano ya Olimpiki mwakani jijini Paris nchini Ufaransa.
Hata hivyo kinachotoa matumaini ni kwamba endapo nyota ya Kipchoge itaanza kufifia, wapo chipukizi wazawa ambao wanaibukia wanaoonekena wametosha kuvaa viatu vya Kipchoge na moja wao akiwa Kiptum.
London Marathon ilikua ni ya pili ambayo Kiptum anashiriki na zote ameibuka mshindi tena akiweka muda bora. Rekodi aliyoiweka mwishoni mwa wiki inamfanya kuwa mtu wa pili mwenye kasi zaidi mbio za marathon.
Aidha katika mbio hizo za London Marathon, alimaliza nusu ya pili (kilomita 21) akitumia muda wa dakika 59 na sekunde 45 ikiwa ni muda bora kuwahi kuandikishwa katika nusu marathon kwenye mbio za marathon kamili.
Huu ni muda bora ukilinganisha na 59:51 aliyoweka Kipchoge katika nusu ya kwanza mbio za Berlin Marathon 2022.
Kiptum alianza kutimka kilomita 30 na kuacha kundi la wanariadha akiwemo Geoffrey Kamworor, Kenenisa Bekele and bingwa wa dunia Tamirat Tola.
Kasi hiyo ya ajabu ya Kiptum ilimfanya amuache kwa dakika tatu bingwa mara mbili wa New York Marathon, Kamworor, aliyemaliza mbio hizo kwa muda wa 2:04:23 naye Tola akishika nafasi ya tatu kwa muda wa 2:04:59.
Macho sasa yatakuwa kwa Kiptum endapo atajitosa mbio za Berlin Marathon Septemba 25 mwaka huu, mbio ambazo zinafahamika kwa rekodi ya dunia kuvunjwa.