Ingwe yapata ushindi wa kwanza Kenya yaizima KCB ya Matano
Muktasari:
- Ingwe ilikuwa haijaonja ushindi wowote msimu huu, lakini kwenye Uwanja wa Ulinzi Sports Complex, jijini Nairobi ilivuna pointi tatu za kwanz katika mechi moja dhidi ya vijana wa Matano ikiwa ni kipigo cha tatu kwa KCB.
MABINGWA wa zamani wa Kenya na Afrika Mashariki na Kati, AFC Leopards 'Ingwe' jioni hii imepata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu (KPL) dhidi ya vijana wa Robert Matano, KCB.
Ingwe ilikuwa haijaonja ushindi wowote msimu huu, lakini kwenye Uwanja wa Ulinzi Sports Complex, jijini Nairobi ilivuna pointi tatu za kwanz katika mechi moja dhidi ya vijana wa Matano ikiwa ni kipigo cha tatu kwa KCB.
Bao la kwanza la AFC Leopards lilifungwa sekunde chache baada ya kuanza kwa pambano hilo kupitia Christopher Koloti lililodumu hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili KCB ilisawazisha nao hilo kupitia kwa Francis Kahiro dakika ya 55, lakini Boniface Munyendo alitupia bao la pili na la ushindi dakika ya 72.
Matokeo hayo yameifanya Ingwe itoke nafasi ya 16 katika msimamo hadi ya saba kwa kufikisha pointi sita kupitia mechi nne, ikilingana na KCB iliyocheza mechi tano inayoshuka kwa nafasi moja kutoka ya saba hadi ya nane.
Ingwe iliambulia sare katika mechi tatu zilizopita, huku KCB ikishinda mbili na kupoteza mara tatu.
Katika mechi nyingine za leo za Ligi hiyo ya Kenya, Kakamega Homeboyz ikiwa nyumbani na kumaliza mechi na wachezaji pungufu ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Ulinzi United, huku Kariobang Sharks ikipasuliwa nyumbani kwa mabao 2-1 na APS Bomet.