INGWE FASTA SOKONI, WALETA MBOGI YA MTU SITA

BAADA ya kuangukia kichapo cha tatu mfululizo wikendi ya hivi majuzi, AFC Leopards waliingia sokoni fasta na kufanya usajili baada ya kuruhusiwa na FIFA.
Soko la usajili lilifungwa rasmi saa sita usiku wa jana Jumatatu lakini hadi kufikia Jumamosi, bado marafuku ya kutofanya usajili dhidi yao haikuwa imefutwa na FIFA.
Hata hivyo baada ya kuiridhishaa FIFA kuwa inaendelea na mchakato wa kuwafidia makocha na wachezaji wake wawili wa zamani iliyowavunjia mikataba pasi na kufuata utaratibu unaotakiwa, waliondolewa kikwazo hicho.
Mara moja Ingwe ilizama sokoni na kuwapata wachezaji sita, ikifanya hivyo kwa haraka kabla ya soko kufungwa usiku wa jana.
Wachezaji hao ni mastraika wawili, mabeki wawili, mlinda lango mmoja na kiungo wa kati wote wakiwa ni wachezaji wa ndani.
Mdokezi kutoka ndani ya klabu anasema watawazindua rasmi wachezaji hao mara tu baada ya FKF itakapowaidhinisha.
"Unajua tumekuwa na ile marufuku ya FIFA na hata usajili huu tumekurupuka tu kuufanya. Imetulazimu kufanya hivyo kwa sasa ila ni mpango tu wa muda mfupi. Ni usajili wa kutushikilia hadi soko lijalo ambapo tutaweza kufanya usajili mwafaka na kwa kuzingatia mapungufu  hususan kwenye timu." Amedokeza afisa mmoja wa Ingwe.
Kocha wa Ingwe, Patrick Aussems alishasema  mapema msimu huu kwamba bila ya kufanya usajili, matokeo yao msimu huu  hatawafurahisha wengi.
Hii ni kwa sababu wamekuwa wakikitegemea kikosi cha wachezaji limbukeni waliopromotiwa kutoka kikosi cha chipukizi baada ya kutokwa na wachezaji 17 wazoefu waliounda kikosi cha kwanza msimu uliopita.
Baada ya kuanza msimu vizuri kwa kuwalima Tusker 1-0, Ingwe wamesajili matokeo mabovu ya mfululizo.|
Walianza na sare tasa dhidi ya KCB, kisha wakalimwa na mashemejio Gor Mahia 1-0 halafu wakafinywa na Bandari 2-1 kabla ya kuumizwa tena na Ulinza Stars 2-0 wikendi.
Kocha Aussems amekuwa akilalamikia ukosefu wa mastraika ila sasa ana nafuu baada ya kusajili wawili.
Safu hii ina taarifa kuwa miongoni mwa mafowadi iliyowasajili ni straika wao wa zamani Kepha Aswani.