Hawa hapa wabaya wa K’Ogalo

BAADA ya mechi tano za Ligi Kuu Kenya msimu mpya, mabingwa watetezi Gor Mahia bado wanaonyesha nia ya kuhifadhi ubingwa wao ila wanapata upinzani mkali kutoka kwa Posta Rangers.
Japo ni mapema mno kutabiri nani ataibuka bingwa wa FKFPL msimu huu, tukumbuke mtaani wanayo msemo wao ‘mapema ndo best’ huku wahenga wakikolezea kwa kusema ‘biashara asubuhi, jioni mahesabu’.
Rangers wanaongoza kwenye msimamo wakiwa na pointi 13 wakiwazidi Gor Mahia na wageni Murang’a Seal kwa pointi nne kila moja.
Vijana hawa wa kocha John Kamau wameamua hawataki kuacha kitu wakishinda mchezo wa nne mfululizo mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kuichapa Kariobangi Sharks bao 1-0 lililofungwa na Peter Otieno.
Rangers inaungana na K’Ogalo zikiwa ni timu mbili pekee ambazo hazijapoteza michezo yao ya ligi kwa msimu huu mpya.
Gor Mahia walikosa fursa kupunguza pengo lao la pointi na Rangers kubaki mbili walipolazimika kutoka nyuma na kusawazisha dhidi ya KCB inayofundishwa na Bernard Mwalala.
Kocha Jonathan McKinstry aliridhika na sare hiyo akisisitiza ni bora wamepata pointi moja kama tatu zimeshindikana wakiendelea kudumisha rekodi yao ya kutofunga msimu huu.
Wakati Rangers na Gor Mahia wakisalia kuwa ‘unbeaten’, magalacticos Kenya Police FC walipata ushindi wake wa kwanza msimu huu chini ya kocha mpya Zdravko Logarusic aliyechukua mikoba ya Francis Baraza.
Mabao ya Kenneth Muguna na Clinton Kinanga yaliwapa ushindi dhidi ya Bidco United waliyopoteza mchezo wao wa kwanza msimu huu kiasi cha kocha Anthony Akhulia kuwawakia wachezaji wake.
Mechi iliyovutia na kuvunja rekodi ya mashabiki kibao kujaza stadi kwa msimu huu ilikua kati ya AFC Leopards dhidi ya Shabana FC kwenye uga wa Ulinzi Complex jijini Nairobi.
Timu zote bado zinasaka ushindi wao wa kwanza na baada ya dakika 90 gemu ilimalizika sare ya bao 1-1 ambapo bao la Ingwe lilipatikana kwa njia ya penalti kupitia Brian Yakhama wakati Peter Ogechi akiisawazishia Tore Bobe.
Nao Sofapaka ambayo pia inasaka ushindi wake wa kwanza msimu huu, imekuwa timu ya pili kumtimua kocha wake raia wa Burundi, Francis Haringingo, kutokana na matokeo mabovu yanayoifanya kusalia mkiani.
Mabingwa hao wa mwaka 2009, wametoa sare moja na kupoteza michezo minne na nafasi ya Haringingo sasa imechukuliwa na Ezekiel Akwana licha ya uongozi awali kukana lengo la kumrudisha Akwan ani kuchukua mikoba ya Mrundi hiyo.