Gor Mahia hali tete

Wednesday July 28 2021
GOR PIC
By Thomas Matiko

MAJI yamewafika Gor Mahia shingoni. Taarifa za utendeti tulizonasa zinaarifu zaidi ya wachezaji 10 wanaounda 'First 11' wanajipanga kuigura klabu hiyo kutoroka msoto.
Nyufa ya kwanza kwenye ukuta wa Gor  ulianza kwa kocha Mreno Carlos Vaz Pinto kuondoka ghafla baada ya kuvunja mkataba wake. Hakuwa amelipwa mshahara wake wa miezi minne kufikia wakati anaondoka.
Kisha akafuata kiungo tegemeo Kenneth Muguna aliyejiunga na Azam FC ya Tanzania halafu beki wao tegemeo Charles Momanyi aliyejiunga na Tusker hivi majuzi.
Sasa hakuna anayetaka kubaki baada ya miamba hao kuondoka huku wachezaji wenzao wa kikosi cha kwanza nao wakijipanga kujitoa. Tatizo kubwa limekuwa suala la  utolipwaji wa mishahara yao.
"Ninaweza kukuhakisha kwamba takriban wachezaji kumi wenzangu wameanza mazungumzo  za kujiunga na klabu zingine. Mawazo yao yapo kwingine kabisa sio Gor tena. Kila mtu anataka kuondoka," kafichua mchezaji mmoja anayeunda kikosi cha kwanza, ambaye naye vile vile yupo kwenye mkakati huo.
Kulingana naye kikosi hakina morali kabisa huku kila mmoja wao mawazo yake yakiwa  kwingine kabisa sababu kubwa utolipwaji wa mshahara wao kwa miezi minne sasa.
"Tumepewa ahadi chungu nzima za kutulipa lakini wapi. KIla siku tunazungushwa tu na menejimenti. Imefikia hataua kwamba hata kupata maji ya kunywa tu wakati wa mazoezi ni tatizo. Sasa kama hiyo imekuwa changamto sembuse  kulipwa fedha zetu," mchezaji huyo kaongeza.
Mpaka sasa Gor hawajashinda mechi zao saba za mwisho za ligi kuu iliyosalia na mechi sita msimu ufike mwisho.
Presha sasa imeanza kumwandama mwenyekiti Ambrose Rachier ambaye ameendelea kugandia uongozini kwa mwaka wa 12 sasa. Vile vile meneja wa timu Jolawi Abondo ambaye kadumu na kikosi hicho kwa zaidi ya miaka saba naye kanyooshewa kidole cha lawama. Sasa mashabiki wanawataka viongozi hawa wajitoe Gor.
Haya yanajiri wakati pia CAF imewakazia Gor kuhusu ushiriki wao wa dimba la Confederation Cup  msimu ujao. Ili kushiriki wanatakiwa kumlipa wing'a Dicsion Ambundo aliyewashtaki FIFA, fidia yake ya Sh1.8 milioni kwa kumvunjia mkataba bila kufuata utaratibu mwafaka. Bado hawajafanya hivyo.
Gor aidha walipigwa marufuku ya kufanya usajili na FIFA kwa sababu ya kushindwa kuwalipa wachezaji wake ilivyowavunjia mikataba yao fidia zao.


Advertisement